Habari za Kitaifa

Shule yatoa hamasisho kuepusha watoto kuuawa mtaani

February 25th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

SIKU chache baada ya kisa cha kushangaza ambapo mtoto mmoja alirushwa na mwenzake kutoka juu ghorofani na kuaga dunia Embakasi, shule moja eneo hilo inatoa hamasisho kwa wanafunzi kuepuka kutangamana na wasiowajua pamoja na walio na michezo hatari.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Quarry katika eneo la Pipeline, Embakasi jijini Nairobi, ameonya wanafunzi dhidi ya kucheza na watoto wasiowafahamu katika mitaa wanayoishi.

Tayari uvumi unaenezwa kuna jini linaloua watoto katika eneo hilo.

Bi Grace Kamau aliambia Taifa Jumapili kwamba huo ni uvumi tu usio na mashiko yoyote.

Badala yake, Bi Kamau aliwataka wazazi na wanafunzi kuwa makini na wanaotangamana nao pale nyumbani na katika mitaa jirani.

“Sijui uvumi huu umetoka wapi lakini binafsi ninahisi ni propaganda za wakora na wahalifu wanaotaka kutumia kisingizio hicho kuvuna pesa kutoka kwa wazazi. Watawadanganya mara ‘tuma pesa mtoto yuko hospitalini’ wakijua fika huo ni uongo,” akasema Bi Kamau.

Alisema tukio la mtoto kurushwa ni la kusikitisha mno na “hatuwezi kulifumbia macho”.

Alisema ni muhimu wazazi kufuatilia kwa makini kujua watoto wao wako salama.

Mapema Februari, familia mzazi aliyejitambulisha tu kwamba anaitwa Mwende, ilimpoteza mtoto wa umri wa miaka mitano baada ya mwenzake kumrusha kutoka ghorofa ya tano hadi chini.

Mzazi aliyejitambulisha ni Bi Mwende ndiye alimpoteza mwanawe. PICHA | FRIDAH OKACHI

“Tulikuwa na mtoto wangu hapo nje. Mtoto mwezake ambaye alikuwa akiendesha baiskeli ndiye alimchukua,” alianza kusimulia Bi Mwende.

Alisema baadaye alisikia nduru akiwa ndani ya nyumba bila kufahamu mwanawe ndiye alikuwa amerushwa.

“Nilisikia kelele huko nje. Mwanzo niliwaza kuwa huenda ni majirani wanapigana jinsi ilivyozoeleka huku,” akaongeza mama huyo.

Lakini alipotoka nje alikutana na jirani ambaye alimuuliza alikokuwa mtoto wake huyo.

“Kwa utaratibu nilimwambia alikuwa na mwezake ambaye sikuwa ninamjua. Nilipoenda kuangalia pale kishindo kilisikika nilishtuka kupata ni mwanangu aliyekuwa amerushwa chini,” akasikitika.

Mtoto aliyeangushwa alipofikishwa katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki, tayari alikuwa amepoteza maisha yake.

Pia visa vingine hatari ni vile ambavyo hutokea na vinavyohusishwa na wapenzi, wachumba au wanandoa kufarakana.

Inadaiwa kwamba baba na mama wanatofautiana, mmoja wao anaweza kumchukua mtoto bila idhini ya mwenzake, hatua ambayo ni hatari kwa sababu hata walimu wanaweza kutiwa hatiani endapo mzazi atakayehisi kuchezewa ngware atataka majibu.