Habari Mseto

Shule za msingi Thika zapata matangi ya maji

May 28th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

SHULE za msingi mjini Thika zimenufaika kwa kupata matangi ya maji ili kukabiliana na janga la Covid-19.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alisema wakati huu taifa linapopambana na homa ya corona ni vyema shule zote za msingi na hata za upili ziwe na maji ya kutosha.

“Kabla ya shule kurejelea shughuli zake ni vyema mikakati iwekwe ili kukabiliana na Covid-19,” alisema Bw Wainaina.

Alisema kati ya shule za msingi 32 mjini Thika, tayari 15 zimefanyiwa ukarabati kupitia fedha za hazina ya maendeleo za NG-CDF.

Alisema amefanya juhudi kuona ya kwamba baadhi ya shule hizo zimepokea matangi ya maji ya lita 10,000 kwa kila moja.

Alipendekeza serikali itathmini kwa makini hali ya mambo kabla ya kuruhusu wanafunzi kote nchini kurejea shuleni.

“Si neno hata shule zikifunguliwa Januari 2021. Aidha si vyema kujipata pabaya ghafla,” alifafanua Bw Wainaina.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina akitandaza sakafu ya darasa mojawapo katika Shule ya Msingi ya Kamenu mjini Thika alipozuru kujionea jinsi inavyofanyiwa ukarabati. Picha/ Lawrence Ongaro

Ameitaka serikali kufanya juhudi kuona ya kwamba walimu wanapokea kiinua mgongo ili kuwapa motisha ya kuchapa kazi kwa bidii.

Baadhi ya shule ambazo tayari zimefanyiwa ukarabati wa kisasa ni Makongeni, Kimuchu, Kiganjo, Kilimambogo, Mbagathi, na Komo.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Mbagathi Bw Muchemi Maguru, alipongeza juhudi za mbunge huyo kwa kujitolea na kuona ya kwamba shule karibu zote za msingi zinafanyiwa ukarabati.

“Wakati shule zitafunguliwa wanafunzi watafurahia mazingira mapya na tutaweza kuwahamasisha ili wawe na ufahamu zaidi kuhusu umuhimu wa kuzingatia usafi kujizuia kuambukizwa homa ya corona,” alisema Bw Maguru.

Alisema kwa muda mrefu shule nyingi za msingi hasa zile za Thika Mashariki zimepata shida ya maji.

“Hapo awali tulitafuta maji hadi mwendo wa kilomita tatu katika Mto Athi. Lakini kwa sasa shida hiyo itakwisha baada ya kupokea matangi ya maji,” alisema mwalimu huyo mkuu.

Alisema kutokana na janga la corona walimu watakuwa na kazi ya ziada kuwahamasisha wanafunzi kila mara kufuata maagizo ya Wizara ya Afya.

Watalazimika kuzingatia kunawa mikono kila mara, kuvalia barakoa, na kuweka nafasi ya umbali wa mita moja hivi kutoka mmoja hadi kwa mwingine.

Hata hivyo, changamoto kubwa ni wanafunzi kuwa wengi katika madarasa na wanapojumuika pamoja wakiwa michezoni na kwingineko.

“Wakati huu ushirikiano unahitajika baina ya walimu na wazazi pamoja na wanafunzi ili kukabiliana na janga hili la Covid-19. Kuna changamoto kubwa bado inayotusubiri,” alisema Bw Maguru.

Naye mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Kilimambogo Bi Philis Kavura Ngige alisema walikuwa wakichota maji kutoka chuo cha walimu cha St Johns Kilimambogo, lakini sasa watajitegemea wenyewe.