Habari Mseto

Shule za wamiliki binafsi zalilia serikali

July 16th, 2020 2 min read

MISHI GONGO na GITONGA MARETE

ZAIDI ya shule 1,000 za wamiliki binafsi nchini huenda zikakosa kufunguliwa mwaka 2021, chama cha shule za wamiliki binafsi nchini (KPSA), kimesema.

Naibu mwenyekiti wa chama hicho, Bw Isaiah Mbaabu, alisema kuna shule 11,000 za wamiliki binafsi nchini, lakini asilimia 10 ya shule zenyewe zimeathiriwa na corona, ikizingatiwa ziko katika majengo ya kukodisha.

Shule hizo zimeajiri zaidi ya wafanyakazi 200,000 ambao tayari wameachwa bila ajira, huku zaidi ya watoto 300,000 wanaotarajiwa kurudi shuleni mwaka 2021, wakiwa hawana pa kwenda.

“Walimu wengi wameacha ualimu na kuingilia biashara nyingine kujipatia riziki. Tumeshindwa kuwalipa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu,” akasema Bw Mbaambu.

Jumatano, wawakilishi wa shule za wamiliki binafsi jijini Mombasa, walilalamika kutengwa katika misaada inayotolewa na serikali ili kuwalinda wasiojiweza katika jamii.

Wawakilishi hao walisema licha ya wao kuwa miongoni mwa wanaotoa huduma muhimu nchini, serikali haijashughulika kuwakinga kutumbukia katika dimbwi la uchochole.

Makahaba

Wakizungumza na wanahabari katika afisi za shirika la Haki Africa, mwenyekiti wa shule za kibinafsi mjini Mombasa, Bw Omar Mboli alisema si sawa watu wa sekta zingine kufadhiliwa na serikali huku wao wakitelekezwa.

“Tunasikitika kuona serikali imetoa ufadhili kwa wasanii, wadau wa sekta ya hoteli, makahaba na kadhalika, ilhali sisi hatujatambulika licha ya kutoa huduma muhimu nchini,” akasema.

Alisema tangu kufungwa kwa shule kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini, walimu wengi wanaohudumu katika shule za wamiliki binafsi wanashindwa kujikimu kimaisha.

Mwenyekiti huyo alisema walimu wa shule za wamiliki binafsi wamesajiliwa katika bodi ya ualimu sawia na wale wa shule za umma. Hivyo wote wanafaa kuangaliwa na serikali.

Bw Mboli alisema tayari wamepoteza walimu watatu mjini Mombasa waliojiua kufuatia hali ngumu ya maisha.

“Juzi mwalimu mmoja alifungiwa nje akiwa na mtoto wa umri wa miezi sita kwa kukosa kulipa kodi ya nyumba. Wako walimu waliojitoa uhai kufuatia kushindwa kukimu familia zao,” akasema.

Alisema tangu kufungwa kwa shule ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona, wamiliki wa shule za uwekezaji wa mtu au watu binafsi wameshindwa kuwalipa mishahara walimu na wafanyakazi wengine katika shule hizo.

Mwenyekiti wa shule hizo katika eneobunge la Mvita, Bw Shadrak Attik, alisema walimu wanapitia hali ngumu ya kiuchumi na wanahitaji msaada wa haraka kutoka kwa serikali.

“Tunahitaji msaada wa haraka,tunashukuru baadhi ya walimu waliajiriwa katika kazi za mtaani,lakini bado kuna wengine hawajabahatika,” akasema.

Aliwasuta viongozi wa serikali kwa kuwakumbuka nyakati za kusaka kura pekee.

“Wakati wanatafuta kura wanakuja kutushawishi na sisi tunawasaidia. Sasa hivi ni sisi tuko katika shida hakuna mtu amejitolea kutusaidia,” akasema.