Shule zafunguliwa changamoto ikiwa kudumisha nafasi kati ya mwanafunzi mmoja na mwingine

Shule zafunguliwa changamoto ikiwa kudumisha nafasi kati ya mwanafunzi mmoja na mwingine

Na SAMMY WAWERU

SHULE kote nchini zimefunguliwa leo Jumatatu, Januari 4, 2021, miezi tisa baada ya kufungwa kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona.

Kenya iliandikisha kisa cha kwanza cha Covid-19 Machi 13, 2020, na ongezeko la maambukizi likailazimisha serikali kuamuru kufungwa kwa shule zote na taasisi za elimu ya juu kama njia mojawapo kuzuia maenezi zaidi.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha mapema Jumatatu ameongoza maafisa kutoka idara ya elimu kukagua shughuli za ufunguzi katika shule mbalimbali.

“Tumeona watoto wanavalia maski vizuri, nyingi zikiwa zilizosambazwa na serikali,” akasema Prof Magoha baada ya kuzuru Shule ya Msingi ya Olympic, jijini Nairobi.

Serikali imetangaza kutenga maski milioni 7.5 zitakazosambazwa kwa wanafunzi ambao wazazi hawana uwezo.

Katika ziara yake Olympic Primary, waziri amekiri kuna changamoto kuafikia kigezo cha umbali kati ya mwanafunzi na mwenzake.

“Walimu na wanafunzi wanahitaji motisha. Tukifanya kazi kwa pamoja tutafanikiwa,” Prof Magoha akasema.

Msongamano wa wanafunzi unatarajiwa kushuhudiwa katika shule za umma, kufuatia kuathirika kwa baadhi ya shule za kibinafsi ambazo hazijamudu mahitaji ya ufunguzi.

Rais Uhuru Kenyatta Desemba 2020 alisema sharti kila mwanafunzi arejee shuleni Januari 2021, akiamuru machifu na manaibu kuhakikisha hakuna mtoto anayesalia nyumbani.

Wanafunzi wapatao 56,000 waliokuwa katika shule za wamiliki binafsi zilizoathirika na mahitaji ya ufunguzi kudhibiti Covid-19, wanahofiwa huenda wakakosa nafasi katika shule za umma.

Waziri Magoha hata hivyo ameagiza shule za umma kupokea watoto waliokuwa katika shule za kibinafsi.

You can share this post!

BBI: Matakwa ya Waislamu kwa Raila

Brian Mandela afunga bao na kusaidia waajiri wake Mamelodi...