Shule zafunguliwa kwa tahadhari

Shule zafunguliwa kwa tahadhari

Na WAANDISHI WETU

AWAMU ya kwanza ya ufunguzi wa shule za msingi na sekondari ilianza rasmi jana ikigubikwa na sintofahamu na tahadhari, miezi saba tangu taasisi za elimu zilipofungwa nchini.

Wengi wa wanafunzi walioripoti shuleni jana ni wa Gredi ya Nne na Darasa la Nane, huku wale wa Kidato cha Nne wakitarajiwa kurudi kwa wingi leo na kesho.

Taasisi zote za elimu nchini zilifungwa mnamo Machi mwaka huu kama hatua ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Wanafunzi wa vyuo wa miaka ya mwisho walirejelea masomo wiki iliyopita.

Mnamo Julai serikali ilitangaza shule zingefunguliwa Januari mwaka ujao lakini ikabadili kauli baadaye ikitaja kupungua kwa maambukizi ya corona nchini.

Katika Kaunti ya Kitui, wanafunzi wengi waliojitokeza shuleni walifukuzwa kwa kufika bila barakoa, ambalo ni hitaji kutoka kwa serikali.

Hii ni licha ya kuwa Gavana Charity Ngilu mnamo Jumapili kuahidi kuwapa wanafunzi wote barakoa.

Katika kaunti ya Mombasa, shule nyingi zilirekodi idadi ya wanafunzi zaidi ya asilimia 50 huku hatua za kiafya za kupambana na maradhi ya Covid 19 zikiwekwa.

Kulingana na uchunguzi wa Taifa Leo katika shule kadhaa, watahiniwa wa Kidato cha Nne na Darasa la Nane walijitokeza kwa wingi, huku wale wa Gredi ya Nne wakiwa wachache.

Idadi ndogo ya wanafunzi wa Gredi ya Nne inahusishwa na wazazi kuhofia usalama wa watoto wao kutokana na umri wao mdogo.

Baadhi ya wazazi wamekuwa wakihofia uwezekano wa watoto wao kuambukizwa virusi wakirudi shuleni.

Matumaini ya wanafunzi kurejelea masomo yalikatizwa katika Shule ya Msingi ya Kathuriri, Kaunti ya Embu kutokana na ukosefu wa vyoo shuleni humo na ikabidi warudi nyumbani.?Katika shule za maeneo ya Msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu, wanafunzi walisalia kutazamana tu baada ya walimu wao kukosa kufika shuleni.

Shule ambazo zilikosa walimu jana ni pamoja na Basuba, Mangai, Milimani, Mararani na Kiangwe.

Masomo katika shule hizo yamekuwa yakitatizika mara kwa mara kutokana na vitisho vya magaidi wa Al Shabaab.

Katika Kaunti ya Nyeri, idadi kubwa ya wanafunzi wa shule za msingi walirudi shuleni. Kati ya shule zilizokuwa na wanafunzi wengi ni Temple Road, Nyamachaki na Muringato.

Akiongoza ukaguzi wa jinsi shule zilivyofunguliwa, Waziri wa Elimu George Magoha alisema Serikali itafuatilia jinsi hali itakavyokuwa kwa madarasa yaliyofungua kabla ya kutangaza wanafunzi wengine kurudi shuleni.

Pia aliwaagiza walimu kutayarisha orodha ya wanafunzi walio na matatizo ya kiafya ili kuwawezesha kupokea huduma za afya haraka, ikizingatiwa wamo kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa corona..

Shule zote pia zimetakiwa kuhakikisha matumizi ya vifaa vya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona kama vile kuvalia barakoa na kutumia vifaa vya kupima joto mwilini yanazingatiwa.

Kuhusu visa vya mimba za mapema ambavyo vimekithiri tangu shule zilipofungwa mnamo Machi, Waziri aliwahimiza wanafunzi walioathiriwa kurejea shuleni huku akiwahimiza walimu kuwasaidia,

Kuhusu karo ya shule hasa kufuatia makali ya Covid-19, serikali imesema kuwa hakuna mtoto atakayefukuzwa kwa kukosa kulipa karo.

Ripoti ya Diana Mutheu, Paul Mutua, Mary Wangari, George Munene, Kalume Kazungu na Regina Kinogu

You can share this post!

Wazee wakemea matamshi ya chuki

Mcheshi Othuol Othuol afariki