Habari Mseto

Shule zafunguliwa mtaala mpya ukitekelezwa

April 29th, 2019 2 min read

OUMA WANZALA na FAITH NYAMAI

SHULE za umma zinatarajiwa kufunguliwa leo huku zikijitayarisha kwa shughuli nyingi kama utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu wa 2-6-6-3. Walimu 5,000 ambao waliajiriwa majuzi na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) pia wanatarajiwa kutumwa katika shule mbalimbali.

Muhula wa pili utaisha mnamo Agosti 2. Muhula wa tatu hautakuwa na shughuli nyingi, ili kuwaruhusu wanafunzi zaidi ya 1.7 milioni kujitayarisha kwa mitihani ya kitaifa.

Walimu wengi wakuu wamelalamikia ongezeko la gharama ya kuendesha shule, wakati mwingine wakiwaomba wazazi kutoa ada fulani ili kuwawezesha kugharamia baadhi ya mahitaji.

Mwezi uliopita, wakuu wa elimu waliiomba serikali kuwaruhusu kuongeza karo shuleni, lakini ikakataa ombi hilo. Hatima ya zaidi ya shule 200 za upili pia haijulikani, kwani bado hazijawasilisha habari muhimu ili kuingizwa katika Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Elimu (NEMIS). Serikali imesisitiza kuwa lazima shule zote zisajiliwe katika mfumo huo ili kupokea fedha kutoka kwake.

Serikali huwa inalipa karo ya Sh22,244 kwa kila mwanafunzi wa shule za upili, huku wale wa shule za msingi wakilipiwa Sh1,420.

Katika muhula kwa kwanza, serikali ilitoa Sh36 bilioni kufadhili mpango wa elimu bila malipo katika shule za msingi na upili.

Katika fedha hizo, Sh30 milioni zilipangiwa kufadhili elimu ya shule za upili, huku Sh6 bilioni zikielekezwa kufadhili mpango wa elimu ya shule za msingi bila malipo.

Fedha hizo zilizolewa baada ya mwezi mmoja, hali iliyozifanya shule hizo madeni mengi.

Hali ya miundomsingi katika shule hizo pia imebaki kuwa changamoto kuu, hasa kutokana na ongezeko la wanafunzi. Hilo ni kufuatia agizo la serikali kuwa lazima kila mwanafunzi anayefanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) lazima ajiunge na shule ya upili. Kulingana na Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili (KESSHA), madarasa katika shule nyingi yamejaa.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha amesema kuwa ashapokea Sh1.5 bilioni kutoka kwa Hazina ya Kitaifa kufadhili uimarishaju wa miundomsingi katika shule hizo.

Serikali inatarajiwa kutoa sehemu ya fedha hizo muhula huu na zile zilizosalia muhula ujao.

Majuzi, Katibu wa Elimu Bellio Kipsang aliiambia K amati ya Bunge Kuhusu Elimu kuongeza mgao wa fedha zinazotengewa shule, akisema kuwa kiasi kinachotolewa sasa hakitoshi.

Huwa tunawatengea wanafunzi Sh1420 katika shule za msingi, huku wale walio katika shule za upili wakitengewa Sh22,244. Fedha hizo hazitoshi,” akasema Dkt Kipsang.’

Kando na hayo, alisema kuwa Sh1.5 bilioni na Sh200 milioni ambazo zilitengewa shule za upili na msingi mtawalia kuimarisha miundomsingi pia hazitoshi.