Habari za Kitaifa

Shule zakosa kufunguliwa baada ya likizo fupi mataifa ya kigeni nayo yakionya raia wao


SHULE zilikosa kufunguliwa Jumanne katika maeneo yaliyokumbwa na maandamano dhidi ya serikali huku mataifa ya kigeni yakionya raia wao kuhusu utovu wa usalama wakiwa Kenya.

Katika eneo la Mlima Kenya, wanafunzi walitumwa nyumbani wasimamizi wa shule wakitaja hofu ya maandamano.

Baadhi ya wanafunzi katika Kaunti ya Laikipia ambao waliratibiwa kurejea shuleni siku ya Jumanne baada ya mapumziko ya katikati ya muhula walishauriwa kusalia nyumbani kufuatia maandamano.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Nanyuki Solomon Koech aliambia Taifa Leo kwamba aliwashauri wazazi wasiwarudishe watoto wao shuleni hadi Jumatano.

“Wanafunzi walipaswa kuripoti Jumanne lakini kwa sababu ya kutokuwa na uhakika kuhusu maandamano yaliyopangwa, tuliahirisha siku ya kuripoti hadi Jumatano,” alisema Bw Koech.

Hali kama hiyo katika Shule ya St Christopher’s, Nanyuki ambapo wanafunzi wataripoti waliopaswa kuripoti Jumanne, wataripoti Jumatano.

Katika Kaunti ya Mombasa, wanafunzi wa shule ya Mbaraki waliagizwa kurudi nyumbani Jumanne asubuhi kutokana na hofu ya maandamano.

Katika Shule ya Upili ya Kisii, tarehe ya kufunguliwa ilisongezwa hadi Jumatano huku katika Kaunti ya Siaya wazazi wakikataa kuruhusu wao kwenda shule.

Jumanne, nchi kadhaa za kigeni zilionya raia wake kuepuka miji mikubwa kutokana na maandamano.

Amerika, Ukraine, Urusi na Poland, ziliwashauri raia wao kuepuka maeneo yenye msongamano wa watu, hasa katikati mwa miji inayoonekana sasa kulengwa na waandamanaji.

“Hata maandamano ambayo yanaonekana kuwa ya amani yanaweza kugeuka kuwa ya vurugu wakati wowote. Maafisa wa usalama wametumia maji ya kuwasha, gesi ya kutoa machozi, na wakati mwingine risasi kukabiliana na maandamano hayo,” taarifa ya Amerika kwa raia wake ilisema.

Taarifa ya RUTH MBULA, MWANGI NDIRANGU, DAVID MUCHUI, MANASE OTSIALO, JURGEN NAMBEKA, KASSIM ANDINASI, STEVE OTIENO NA KEVIN CHERUIYOT