Habari Mseto

Shule zilizoathirika kukosa kufunguliwa

May 10th, 2024 1 min read

NA MERCY SIMIYU

SHULE zinapofunguliwa Jumatatu kwa muhula wa pili uliocheleweshwa, serikali imetangaza kuwa baadhi ya shule katika kaunti saba hazitarejelea masomo yake.

Akizungumza alipozuru shule sita jijini Nairobi, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alitangaza kuwa, baadhi ya shule katika kaunti saba ikiwemo Tana River, Homa Bay, na Kisumu, huenda zisirejelee shughuli zake Jumatatu.

Aidha, Bw Machogu aliwahimiza wazazi katika shule zilizoathirika kuwa na subira. Aliwahakikishia kuwa kalenda ya muhula itarekebishwa ili kuwasitiri watoto wao akisema mvua kubwa imeathiri kaunti zilizotajwa.

“Majina ya shule zilizoathiriwa yatafichuliwa hivi karibuni. Hata hivyo, inatarajiwa kuwa asilimia mbili (2) ya shule zilizopo Kisumu, Homabay, na Tana River huenda zisifunguliwe kutokana na mvua kubwa inayoendelea kuathiri eneo hilo pakubwa. Juhudi zinatekelezwa kuwezesha mchakato laini wa uhamisho. Isitoshe, mbinu za masomo mbadala zitaangaziwa ili kuhakikisha elimu inaendelea katika shule hizi chache zinazojumuisha chini ya asilimia tano ya idadi yote,” alisema.

Kaunti zilizoathirika zinajumuisha Busia, Tana River, Homa Bay, Baringo, Kisumu, Nakuru, na Kirinyaga miongoni mwa nyingine.