Habari za Kitaifa

Shule zilizogongwa na mafuriko kuchelewa kufunguliwa – Dkt Kipsang

April 27th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

HUENDA serikali ikachelewesha kufunguliwa kwa baadhi ya shule katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko nchini, kulingana na Wizara ya Elimu.

Hata hivyo, Katiba katika Wizara hiyo anayesimamia Idara ya Elimu Msingi Belio Kipsang mnamo Ijumaa alisema kuwa shule zitafunguliwa jinsi ilivyoratibiwa katika kalenda ya masomo.

“Kwa mfano katika Kaunti ya Nairobi, kuna jumla ya shule 64 ambazo zimeathiriwa pakubwa na huenda tukachelewesha kufunguliwa kwa shule hizo,” Dkt Kipsang akasema.

Alisema hayo wakati wa Mkutano wa Kamati ya Kiufundi ya Kitaifa ya Kupambana na Majanga.

Mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi kutoka wizara mbalimbali za serikali, ulioongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi.

Dkt Kipsang alitoa hakikisho kuwa Wizara ya Elimu itashughulikia mahitaji ya shule zote zilizoathirika na mafuriko na athari nyingine za mvua kubwa inayoshuhudiwa kote nchini.

Kulingana na kalenda ya masomo, shule zote za msingi na za upili zitafunguliwa kwa muhula wa pili mnamo Aprili 29, 2024.

Kamati hiyo kuhusu majanga inalenga kuratibu mikakati iliyowekwa ya kupambana na athari za mvua hii ya El Nino.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na magavana wa kaunti mbalimbali na wawakilishi kutoka Chama cha Sekta ya Kibinafsi Nchini (Kepsa).

Baadhi ya shule katika maeneo ya Budalang’i (Busia) na Kano (Kisumu) zinatumika kama hifadhi kwa watu ambao nyumba zao zilisombwa na mafuriko.