Shule zinapofunguliwa tuwe waangalifu Covid-19 isitulemee – Kagwe

Shule zinapofunguliwa tuwe waangalifu Covid-19 isitulemee – Kagwe

Na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe amesema kuna uwezekano wa ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini kushuhudiwa shule zitakapofunguliwa katika kipindi cha siku chache zijazo.

Shule zote na taasisi za elimu ya juu nchini zitafunguliwa mnamo Jumatatu, Januari 4, 2021.

Bw Kagwe amesema Ijumaa ongezeko la visa vya Covid-19 huenda likachangiwa na ufunguzi wa shule, ikizingatiwa serikali imeamuru watoto wote nchini warejee shuleni.

Hata hivyo, Waziri aliashiria kuwa upungufu wa maambukizi hayo utaanza kushuhudiwa mwezi Februari, akisisitiza serikali imeweka mikakati maalum kuhakikisha wanafunzi wanalindwa dhidi ya kuambukizwa.

“Walimu wawe makini na waangalifu sana. Hatutaki kupoteza mwalimu wala mwanafunzi yeyote, tutahakikisha kila mtu ni salama,” akasema.

Aidha, Bw Kagwe amehimiza wazazi kuhakikisha wanao wana maski za kutosha, akipendekeza wawe na zaidi ya mbili zinazoweza kuoshwa na kutumika tena.

“Tunaambia wazazi maski ihesabike ni sare ya shule,” akasema.

Waziri hata hivyo alisema serikali itasaidia wasio na uwezo, kuhakikisha wamepata barakoa (maski). Alisema serikali imeweka pembezoni maski zipatazo milioni 7.5 kwa minajili ya shughuli hiyo.

Bw Kagwe amesema hayo wakati akihutubia wanahabari Afya House, Nairobi, baada ya kutia saini mkataba wa makubaliano na matabibu na maafisa wa kliniki kurejea kazini, ambao wamekuwa kwenye mgomo wa kitaifa.

Juma lililopita, madaktari walisitisha mgomo wao baada ya kuafikiana na serikali kuhusu matakwa yao.

Wauguzi ndio wamesalia kwenye mgomo, Waziri Kagwe akisema mazungumzo ya muafaka na wawakilishi wa muungano wa kuwatetea, KNUN, yanaendelea.

Katika kikao tofauti na wanahabari Nairobi, Waziri wa Elimu Prof George Magoha alisema serikali imejiandaa kwa minajili ya shule kufunguliwa Januari 4.

Kufikia Ijumaa, maambuzi mapya 156 yalithibitishwa kutoka kwa sampuli 4,317 chini ya saa 24 zilizopita, huku 11 wakiangamia.

Jumla ya visa 96, 614 vya maambukizi ya corona vimeandikishwa nchini tangu kisa cha kwanza kitangazwe mnamo Machi 2020, idadi ya waliofariki kutokana na virusi hivi hatari ikigonga 1,681.

Aidha, jumla ya sampuli 1,050,984 zimefanyiwa ukaguzi na vipimo.

You can share this post!

Cavani apigwa marufuku na kutozwa faini ya Sh14 milioni kwa...

Wakenya kupokea kwa hiari chanjo ya Covid-19