Habari Mseto

Shule zisizopaka mabasi yao rangi ya manjano kuona cha moto

April 2nd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

SERIKALI itayatwaa mabasi yote ambayo hayatakuwa yamepakwa rangi ya manjano kuanzia Jumanne.

Waziri msaidizi wa Elimu Bw Simon Kachapin alisema Wizara ya Elimu itashirikiana na mamlaka ya kitaifa ya usafiri na usalama (NTSA) na maafisa wa idara ya polisi kutekeleza agizo hilo la kukamatwa kwa mabasi yote ambayo hayajapakwa rangi ya manjano.

Maafisa wakuu wa Wizara ya Elimu pamoja na wale wa kaunti wanapaswa kuhakikisha kila basi la shule limepakwa rangi ya manjano kufikia Machi 31.

Jumapili ilikuwa siku ya mwisho kwa mabasi yote ya shule za upili na zile za msingi zilizo na mabasi kupakwa rangi ya manjano.

“Serikali haitaongeza muda wa kupaka mabas rangi hiyo ya jano. Shule zote zapasa kutekeleza agizo hilo lililotolewa mwaka jana,” alisema Bw Kachapin.

Awali katibu mkuu wa elimu Bw Belio Kipsang aliwaagiza walimu wakuu wahakikishe mabazi yote yamepakwa rangi hiyo.

Akizugumza katika shule ya Upili ya Wavulana ya St Peters eneo la Mumias wakati wa mkutano mkuu na wazazi, Bw Kachapin alisema wakuu wa shule za sekondari wanaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua kali na idara husika.

 “Ingawa shule nyingi zimetekeleza agizo hilo, kungali na shule chache ambazo hazijaitekeleza zikidai hazina fedha za kupaka rangi mabasi yao,” alisema.

Agizo hilo lilitolewa Januari 2017 na aliyekuwa Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i.