Akili Mali

Si lazima nyuki kufugwa msituni; fahamu uzalishaji asali mjini

May 25th, 2024 2 min read

NA PATRICK KILAVUKA

MADHUMUNI ya kustawisha ufugaji nyuki katika Shule ya Msingi ya Tumshangilieni Mtoto, Nairobi yalikuwa kuzalisha asali ya kutosha kwa matumizi ya wanafunzi wanaolelewa na skuli hii kuinua kiwango cha virutubisho vyao kuhimili magonjwa mbali na kuuza ili kustawisha kituo cha ufunzaji wa ufugaji wa nyuki.

Mahitaji ya asali ni mengi kwani inaweza kutumiwa katika uji, chai, usindikaji na kadhalika.

Mkulima mfugaji wa nyuki Emmanuel Juma aliye pia meneja ya kilimo katika shule hiyo, alishawishika kuanzisha ufugaji huu mwaka wa 2020 hususan wakati asali ilihitajika kwa wingi wakati wa corona.

Kwa vile alikuwa amejifunza kuhusu ufugaji wa nyuki akiwa Chuo cha Kilimo cha Baraka Agriculture, Nakuru na kufuzu na stashahada ya Kilimo, alitumia maarifa hayo kuanzisha mradi huo shuleni humo baada ya kuajiriwa kama meneja wa ukulima.

Emmanuel anasema alianza ufugaji na mizinga minne pekee na sasa ameongezea kuwa kumi na miwili kwani mahitaji ya asali yanazidi kuongezeka.

Wakati huo, anasema alivuna lita 30 za asali na kuuza kila lita Sh850 – 1,000 kulingana na soko.

Sasa anatarajia kuvuna karibu lita 110 – 120 kutoka kwa mizinga aliyostawisha. Anauzia maduka na watu binafsi baada ya kutoa ambayo hutumiwa shuleni.

Je, unahitaji nini kustawisha ukulima huu?

Emmanuel anasema kwanza kabisa si lazima nyuki kufugiwa msituni bali nyuki zinahitaji uwepo wa mizinga faafu na mahali tulivu.

Hata hivyo, inafaa kuwa mahali mimea au miche ambayo ni chanzo ya kupata nta kama malighafi ya kutengenza asali inapatikana.

Inahitaji pia kuwa mbali na barabara, majengo, viwanda kuepukana kelele, uviziaji au kemikali za viwandani kuathiri nyuki wakati wa kutengeneza asali.

Yeye hutumia mizinga ya Longstroth kutokana na mizinga hii kuwa na mahali pa malkia kukaa na pengine pa kutengenezea asali.

Pia, huwa rahisi kuvuna asali katika mzinga wa Longstroth kuliko Topbar pasi na kuvuruga mahali panapokaa malkia na kutatiza uzalishaji wa asali. Kando na Topbar ina sehemu moja ambako hukaa malkia na kuzalishia asali pia.

Emmanuel anasema miezi mizuri ya kustawisha ufugaji wa nyuki ni Januari, Februari na Machi kwani huu ndio wakati malkia wa nyuki huwa wanahama sehemu moja hadi nyingine kujenga himaya mpya kwani malkia hawawezi kufugika katika mzinga mmoja na hivyo basi, mmoja huhama kujitafutia mzinga kujitawala.

Mahali pa kuangika mzinga panategemea na uwepo wa nyuki na upatikanaji wa nta kuunda asali. Inachukua mwezi mmoja au miwili mzinga kuhamiwa ikiwa unawekwa au kuangikwa mahali pazuri.

Baada ya kuhamiwa mzinga na nyuki, huchukua miezi mitatu au minne kuvuna asali.

Kabla kuvuna asali, Emmanuel anasema unafaa kukagua masega kwa kutumia kifaa cha ukaguzi kuangalia kama asali unataka kuvuna imekomaa au imejaza vilivyo.

Aidha, unahitaji vifaa vingine kama mabuti, suti ya kujikinga, glavu na kidude cha kufukiza moshi ambacho hutumia kutuliza nyuki wakati wa kuvuna.

Changmoto tu ya ufugaji nyuki ni mnyama aitwaye Njegere (honey badger) ambao hupakua asali na masega na mchwa mweusi (black ants) ambao huvamia nyuki japo wanaweza kudhibitiwa kwa kuweka jivu au Dududust na mafuta chini ya miti ambako mizinga imeangikwa.