Makala

‘Si lazima ukate miti ndipo uchome makaa’

March 28th, 2018 2 min read

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA enzi hizi ambapo kumekuwa na uharibifu wa mazingira kwa sababu ya ukataji miti, anatoa suluhu kwa kuunda makaa kutokana na uchafu wa makaa na taka.

Ni kazi ambayo Stella Sigan, 35, amekuwa akiifanya kwa miaka mitatu sasa kupitia mradi wake wa Alternative Waste Technologies-AWT ambapo bidii yake imesaidia kukuza mazingira kwa kutumia uchafu vilevile kupunguza ukataji miti kutengeneza makaa.

Makaa haya kwa jina briquettes hutengenezwa kwa vumbi ya makaa na taka ambapo tangu waanze mwaka wa 2015, wametumia zaidi ya tani 600 za uchafu huo.

Mbali na kusafisha mazingira, yakilinganishwa na kuni, makaa haya yanawaka kwa muda mrefu na kutoa moshi mchache. Pia ni ya bei nafuu huku wateja wake wakiwa nyumba binafsi, taasisi za kielimu, hoteli na mikahawa

Kwa kawaida yeye hununua vumbi ya makaa kutoka kwa wakazi wa Kibera ambapo wanatengeneza kati ya mifuko 200 na 300 ya makaa haya kila mwezi.

Kwa sasa anafanya kazi na kikundi cha watu sita wanaohusika na shughuli za kuunda makaa haya na wengine takriban 100 wanaokusanya taka na uchafu wa makaa unaotumika katika shughuli hii huku wengine sita wakiyasambaza kwa wateja.

Alihitimu na shahada ya uundaji mavazi na mapambo ya nyumbani kutoka Chuo Kikuu cha Egerton. “Nikiwa chuoni, penzi langu la ujarisiamali lilijitokeza huku nikianzisha biashara ya ushonaji nguo na mapambo ya nyumbani, lakini kwa bahati mbaya biashara hiyo haikudumu,” asema.

Ili kuimarisha ujuzi wake kibiashara, alisomea shahada ya uzamili katika masuala ya kiuchumi na biashara na pia kujiunga na mpango wa Young African Leadership Program, mpango wa kutoa mafunzo ya biashara, ujarisiamali na uongozi miongoni mwa vijana kutoka mataifa 14 ya Afrika ambapo alipiga msasa ustadi wake wa kibiashara.

Penzi hili lilimjia alipokuwa akifanya kazi katika shirika la Carolina for Kibera, kama afisa anayesimamia masuala ya kiuchumi na ujarisiamali.

Ni hapa ndipo alipata wazo la kuanza kuunda makaa haya. Mwanzoni jitihada zake kuuza bidhaa hii hazikufaulu na akaamua kufanya utafiti zaidi kutuma maombi ya kupata ufadhili.

Mwaka wa 2016, alikuwa mmojawapo ya wajarisiamali 1,000 walionufaika na ufadhili wa Wakfu wa Tomy Elumelu ambapo alipokea mafunzo, unasihi wa kibiashara bali na kupokea mtaji wa shilingi laki tano alizotumia kuanzishia biashara hii.

Lakini ari yake kamili ilimjia kutokana na nia yake ya kutaka kuimarisha maisha ya raia wa kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Eneo hili huwa na idadi kubwa ya vifo vya mama na watoto kutokana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na moshi wakati wa mapishi. Na nilipata taswira kamili ya masaibu yao baada ya kuingiliana na wakazi wa vitongoji duni na hasa Kibera,” aeleza.

Kabla ya kuanzisha biashara hii alifanya majaribio kwa kuyanunua kutoka kwa wafanyabiashara ambao tayari walikuwa wanayaunda na kuwauzia wakazi Kibera.

Kwa sasa nia yao ni kupanua huduma zao hadi magharibi mwa Kenya ambapo wanapanga kuanzisha kiwanda cha kutengeneza makaa haya.