Makala

Si lishe tu, kilimo cha 'minji' kinaongeza rutuba shambani

November 12th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Kwa muda mrefu David Muriuki ambaye ni mtaalamu na afisa wa Kilimo Kaunti ya Kirinyaga amekuwa akijaribu kuangazia suala la udongo shambani.

Akilinganisha hali ya sasa ya udongo na ile ya zamani, anakiri kuna tofauti kubwa, tofauti ambayo imechangia kuwepo kwa magonjwa yanayosababishwa na tabiamlo.

Ugonjwa hatari wa Saratani, umekuwa ukihusishwa na namna au jinsi watu wanakula, hususan chakula kilichosindikwa na vilevile mazao ya kilimo yaliyolimwa kwa kutumia fatalaiza ama dawa zenye kemikali.

Mtaalamu Muriuki anaonya kuwa wakulima wasipobadilika na kukumbatia mfumo wa kilimohai kuzalisha mazao, magonjwa yanayohusishwa na lishe yataendelea kushuhudiwa.

Saratani ni gonjwa hatari ambalo linaendelea kuangusha wakubwa kwa wadogo, wembamba kwa wanene, maskini kwa matajiri…na mojawapo ya njia kulidhibiti ni kula chakula salama.

Matumizi ya fatalaiza na dawa zenye kemikali zinaendelea kudhoofisha mashamba, Muriuki akisema baadhi ya migunda Kirinyaga ni kati yamo.

Huku akifahamu bayana athari za pembejeo hizo, mtaalamu huyu amekuwa katika mstari wa mbele kuhamasisha wakulima kukumbatia mfumo wa kilimohai ili kunusuru udongo.

“Awali, nikitumia mfano wa mimea kama vile ndizi, mahindi na nyanya, mazao yalikuwa mengi na salama, ila wakulima walipotekwa nyara na matumizi ya fatalaiza na dawa zenye kemikali kuongeza mazao, wanayapata kwa muda mfupi, kisha yanapungua.

David Muriuki mtaalamu na afisa wa kilimo Kirinyaga anashauri wakulima kurejelea mfumohai ili kunusuru hadhi ya udongo. PICHA/ SAMMY WAWERU

“Wasipotumia pembejeo zenye kemikali shamba halitazalisha wanavyotaka. Hii ina maana kuwa udongo umedhoofika na kuwa dhaifu. Ni hatari kwa wanaokula mazao hayo,” anafafanua mdau huyo.

Kama mtaalamu na mhudumu katika sekta ya kilimo, amekuwa akijaribu juu chini kuhimiza wakulima kurejelea matumizi ya mbolea ya mifugo na pia kuku ili kunuru mashamba.

“Kuna baadhi ya kampuni au mashirika ya kilimo yanayotengeneza mboleahai na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa zisizo na kemikali, wakulima watumie pembejeo zao na serikali iwapige jeki waundaji hao,” anashauri.

Huku wadau katika sekta ya kilimo wakipuliza kipenga na kuhamasisha haja ya kudumisha hadhi ya mashamba yetu, suala la mzunguko wa mimea shambani (crop rotation) ni muhimu.

Kigezo hiki kinaenda sambamba na kuimarisha rutuba. Timothy Ngugi, ambaye mbali na kuwa mtaalamu wa zaraa, pia ni mkulima nguli wa mimea inayochukua muda mfupi kuzalisha, anasema njia pekee kuimarisha rutuba udongoni ni kupitia upanzi wa maharagwe asilia aina ya njegere, maarufu kama ‘minji’.

Yakiwa yanaorodheshwa katika Familia ya Legumi, kulingana na Ngugi, njegere ni mimea iliyosheheni Nitrojini, madini muhimu katika shughuli za kilimo. “Ukitaka kuongeza Nitrojini shambani, usitumie fatalaiza, panda njegere au maharagwe ya kawaida,” anahimiza.

Sawa na Ngugi, mkulima Martin Mwenda anaungama kuwa maharagwe hayo yana tija chungu nzima shambani, hasa katika kuimarisha rutuba.

Mwenda ni mkulima hodari wa ngano na viazi eneo la Timau, Kaunti ya Meru, na anasema baada ya kufanya mavuno hupanda njegere. Ana zaidi ya ekari 20.

“Hufanya mzunguko wa mimea kwa kutumia minji kuongeza rutuba kwenye udongo. Hata ingawa hutumia fatalaiza kunawirisha mazao, huwa situmii yenye kemikali,” Mwenda anaelezea.

Njegere, kando na kuwa mimea yenye manufaa tele kwa mashamba, mazao yake yana mapato ya haraka. “Ekari moja huzalisha takriban tani nne, sawa na kilo 4, 000,” mkulima huyo anadokeza.

Aidha, wakati soko limenoga, kilo moja hununuliwa kati ya Sh80 – 100. Haipungui Sh40 kwa kilo soko likiwa duni.

Kulingana na mkulima huyo, maharagwe hayo hayana gharama kuyakuza, kwani hutumia mbolea ya mifugo. Changamoto zake ni shambulio la wadudu pekee na magonjwa yanayoathiri maharagwe, ingawa ni nadra kushuhudiwa.

Yanachukua chini ya miezi minne pekee kuzalisha mazao, baada ya upanzi.