Michezo

Si wakati wa kuwazia kuvunja rekodi za Guardiola EPL – Klopp

July 6th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Jurgen Klopp wa amesema ingawa matamanio makubwa ya Liverpool kwa sasa ni kuvunja rekodi za Manchester City, ni mapema sana kwa vijana wake kuanza kuwazia ufanisi huo.

Ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Aston Villa mnamo Julai 5, 2020 uliendeleza rekodi yao ya kutopoteza wala kuambulia sare katika mechi zote 17 za hadi kufikia sasa msimu huu uwanjani Anfield.

Liverpool ambao mabao yao yalifungwa na Sadio Mane na chipukizi Curtis Jones, kwa sasa wanajivunia alama 89 kutokana na mechi 33.

Masogora hao wa Klopp wanahitaji sasa alama 12 pekee kutokana na mechi tano za mwisho wa msimu huu ili kuivunja rekodi ya Man-City waliojizolea jumla ya alama 100 katika msimu wa 2017-18.

“Tumekuwa tukimakinikia kila mchuano kwa wakati wake. Sidhani hilo litabadilika. Iwapo tutavunja rekodi kwa kufanya hivyo, ifahamike kwamba hatukuwahi kuandaa kikao na kuafikiana kwamba tuna ulazima wa kufanya hivyo,” akatanguliza kocha huyo mzawa wa Ujerumani.

“Tutaanza kuwazia rekodi baadaye. Pengine msimu huu, au muhula ujao kwa kuwa tutalenga zaidi kufanya mambo makubwa spesheli,” akaongeza.

Mbali na kuweka rekodi mpya kwa kuzoa alama nyingi zaidi katika msimu mmoja wa EPL na kukamilisha kampeni za muhula huu wakijivunia pengo kubwa zaidi kati yao na nambari mbili Man-City, Liverpool pia wana uwezo wa kufikia rekodi ya miaka 128 ya Sunderland waliokamilisha msimu kwa kushinda mechi zao zote za nyumbani.

Kufikia sasa, Liverpool wamesajili ushindi katika mfululizo wa mechi 24 uwanjani Anfield tangu walazimishiwe sare ya 1-1 na Leicester City mnamo Januari 2019.

Mechi dhidi ya Villa ilikuwa ya kwanza kwa Liverpool kutandaza uwanjani Anfield tangu kutawazwa mabingwa wa taji la EPL. Ni matarajio ya Klopp kwamba vijana wake sasa watapata hamasa ya kukamilisha kampeni zilizosalia kwa matao ya juu zaidi baada ya kuweka kando maruerue ya kichapo cha 4-0 kutoka kwa Man-City mnamo Julai 2, 2020.

Chini ya kocha Dean Smith, Villa kwa sasa wamepoteza mechi tatu kati ya tano zilizopita tangu kurejelewa kwa kipute cha EPL mnamo Juni 17, 2020. Kichapo kutoka kwa Liverpool kilididimiza zaidi matumaini yao ya kusalia ligini kwa minajili ya msimu ujao.

Villa kwa sasa wanashikilia nafasi ya 18 kwa alama 27 sawa na Bournemouth. Ni pego la alama sita ndilo linatamalaki kati yao na Norwich City wanaovuta mkia.

Liverpool watakuwa wageni wa Brighton uwanjani American Express mnamo Julai 8, 2020 huku Villa wakiwaalika Manchester United siku moja baadaye.