Makala

Si Yavi tu, hawa hapa wanariadha wengine waliopiga teke Ukenya kukimbilia nchi nyingine

August 8th, 2024 3 min read

KENYA inatambulika sana katika ulimwengu wa riadha. Ni kawaida kwa raia wa Kenya ughaibuni kuulizwa mara kwa mara kama wao ni wakimbiaji.

Mwanariadha mzaliwa wa Kenya wa hivi karibuni zaidi kuzolea taifa jingine sifa ni Winfred Yavi.

Mwaka wa 2023, Yavi alisema alijaribu kuwakilisha Kenya mara kadhaa bila mafanikio.

Yamkini, kikubwa kinachovutia wanariadha hawa kuwakilisha nchi nyingine ni malipo ya mamilioni ya pesa pamoja na marupurupu.

Winfred Yavi – Bahrain

Alitunukiwa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji mnamo Jumanne Agosti 6, 2024 katika Makala ya Olimpiki ya Paris 2024 nchini Ufaransa.

Katika mashindano haya, Mkenya Faith Cherotich, mwenye umri wa miaka 20, aliibuka wa tatu na kupokea medali ya shaba.

Malkia huyo wa riadha mzaliwa wa kaunti ya Makueni, anawakilisha taifa la Bahrain.

Nchi hii inawekeza kwa wanariadha ili kuboresha hadhi yao katika sekta ya michezo hii.

Mkimbiaji Winfred Yavi aliposhinda mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji akiwakilisha Bahrain baada ya kuacha uraia wa Kenya. Picha|Joan Pereruan

Ruth Jebet – Bahrain

Mnamo mwaka wa 2013, Ruth Jebet alihiari kupata uraia wa Bahrain akiwa na umri wa miaka 16.

Mkimbiaji huyo wa mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji, alizaliwa Novemba 17, 1996.

Alikuwa mshikilizi wa rekodi ya dunia pamoja na kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki 2016, kabla ya kugonga umri wa miaka 20.

Zaidi ya haya, alishinda mbio za Diamond League mara mbili na mara moja katika mashindano ya bara Asia – Asian Games.

Eunice Jepkirui Kirwa – Bahrain

Miaka mitatu kabla ya Jebet kuwakilisha Bahrain, Eunice Jepkirui alikuwa amemtangulia.

Jepkirui aliwakilisha Kenya katika maisha yake ya ujana kabla ya kuenda Bahrain.

Mwaka wa 2016 katika Olimpiki ya Rio de Janeiro, Jepkirui alishinda medali ya fedha.

Vile vile, alitunukiwa nishani ya shaba katika mashindano ya Riadha ya Dunia na kutamba katika mbio za Asia – Asian Games.

Lakini ushiriki wake katika michezo ulikumbwa na vikwazo baada ya kupigwa marufuku kwa tuhuma za kutumia dawa za kututumua misuli.

Stephen Cherono – Qatar

Mwanariadha huyu alikuwa ameweka Kenya kwenye ramani ya dunia lakini alipofika umri wa miaka 20, alikimbilia uraia wa Qatar 2023.

Mwaka wa 2002 katika michezo ya jumuiya ya madola, jijini Manchester Uingereza, Cherono alishindia Kenya nishani ya dhahabu katika mbio za kuruka viunzi na maji za mita 3000.

Hapa, alivutwa na mnofu mkubwa wa zaidi ya shilingi laki moja kwa mwezi katika maisha yake ya uhai.

Kuendana na matakwa ya mamlaka ya Qatar na makubaliano yao na Kenya, mwanariadha huyu alibadili jina na kuitwa Saif Saaeed Shaheen.

Saif ni bingwa mara mbili wa dunia wa mbio za kuruka viunzi na maji mita 3000.

Leonard Korir – USA

Mkimbiaji wa mbio za masafa marefu Leonard Korir alihamia uraia wa Amerika (USA) baada ya kupata ufadhili wa elimu ya chuo nchini humo.

Haya yalijiri mnamo Septemba 2009.

Mbali na kuchochewa na kisomo ughaibuni, uhamisho huu ulikuwa na mvuto wa miundomsingi ya hali ya juu ya michezo.

Alitamba katika mbio nyingi na kuvuma zaidi alipokata utepe wa mbio za masafa marefu jijini New York 2016.

Katika nusu marathon ya New York mwaka huo, Korir aliweka mkobani medali ya dhahabu.

Lonah Chemtai Salpeter – Israel

Mwanariadha Lonah Chemtai Salpeter Alitamba katika mbio kadhaa za masafa marefu na za umbali wa kadri.

Hii ilikuwa kabla ya  kutema kuwakilisha taifa alikozaliwa na kukumbatia uraia wa Israel 2016.

Kivyake, Lonah aliona haja ya kuhamia Israel kuishi na mume wake, lakini jeki aliyopata kutoka kwa shirikisho la riadha la nchi hiyo lilimpa msukumo zaidi.

Chemtai ni bingwa mara moja wa mashindano ya Ulaya (Berlin, 2018).

Pia alishinda medali ya shaba katika mbio hizo za masafa marefu Ulaya (Munich 2022).

Kadhalika, ameweka kibindoni nishani kadhaa katika mashindano ya masafa marefu ya dunia.

Alivaa medali ya dhahabu ya mbio za masafa marefu za Tokyo Marathon 2020.

Na mwaka wa 2022, Lonah aliibuka wa pili na kunyakua nishani ya fedha aliposhiriki New York Marathon.

Vile vile Israeli ilijivunia medali ya shamba mwanariadha huyu alipopata nafasi ya tatu katika mbio za Boston Marathon 2023.

Bernard Kipchirchir Lagat – USA

Bernard Kipchirchir Lagat alifana sana alipowakilisha Kenya kati ya mwaka wa 2000 na 2004.

Alikuwa kwenye jukwaa la nishani duniani aliposhinda shaba katika mbio za  mita 1500 wakati wa Olimpiki za Sydney 2000.

Mwaka wa 2004, alishinda medali ya fedha katika Olimpiki ya Athens, Ugiriki.

Lakini ilipofika Machi 2005, Lagat akawa raia wa USA. Lilikuwa tukio lililowaacha Wakenya wengi kinywa wazi.

Anne Wafula – Uingereza

Licha ya kuwa mlemavu akiwa mchanga, Anne Wafula alifuata ndoto yake ya riadha hadi akatambuliwa.

Mnamo mwaka wa 2004 jijini Athens, Ugiriki, Wafula aliwakilisha Kenya katika mbio za viti vya magurudumu.

Haya yalikuwa mashindano ya wanamichezo walemavu ya Paralympics ya umbali wa mita 400.

Mwaka wa 2006 aliamua kuwa raia wa Uingereza ili aishi na mume na mwana wake.

Nyakati hizi aliingia katika vikosi vya michezo yanayohusisha watu walemavu Team Britain.