HabariSiasa

Siasa kanisani zapigwa marufuku

September 10th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

ASKOFU wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Murang’a, amepiga marufuku wanasiasa dhidi ya kuhudhuria ibada kwenye makanisa yake, kutokana na zogo lililotokea Jumapili kati ya wabunge Ndindi Nyoro na Maina Kamanda.

Kulingana na ilani iliyotumwa na Askofu James Maria Wainaina, makasisi wote wameagizwa kufutilia mbali mialiko yote ya harambee kwa wanasiasa, akisema tukio la Jumapili limeaibisha kanisa hilo. Askofu Wainaina pia alishutumu ghasia katika kanisa la Gitui.

“Habari za jioni ndugu makasisi. Wengi wenu mnafahamu kilichotokea katika parokia ya Gitui. Sisi sote tumeaibika ndiyo maana ningependa kuwajuza kwamba mfutilie mbali mialiko yote ya wanasiasa katika makanisa yenu,” akasema kwenye ujumbe huo.

Kasisi huyo ambaye alizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu alisema kisa cha Jumapili hakikufaa kutokea japo akakiri kwamba hajajuzwa na kasisi wa kanisa hilo kuhusu tukio hilo.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba tukio hilo lilifanyika katika kanisa letu. Sikuwa na habari kwamba kulikuwa na wageni ambao walialikwa kwenye kanisa hilo na nilisikia tu kupitia vyombo vya habari kwamba ghasia zilikuwa zimetokea. Ni jambo la kutamausha na nimeanza uchunguzi kulihusu kabla ya kuchukua hatua,” akasema Askofu Wainaina.

Mkuu wa kanisa hilo nchini Kadinali John Njue, amewatwika jukumu Maaskofu wa Parokia mbalimbali, kuamua iwapo viongozi wanaohudhuria ibada kwenye maeneo yao, wataruhusiwa kuwahutubia waumini au la kama njia ya kuzuia ghasia kati ya wanasiasa wa mirengo mbalimbali.

Kadinali Njue alisema ni maaskofu hao ambao wanaelewa hali ya kisiasa katika parokia wanazosimamia kwa hivyo wao ndio wanafahamu njia ya kukabiliana na joto la kisiasa linalozidi kupanda kwenye maeneo hayo.

Askofu huyo alitoa tangazo hilo baada ya tukio la Jumapili ambapo Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro na Mbunge Maalum Maina Kamanda, walikabiliana kanisani kuhusu nani alifaa kuwa mfawidhi kwenye hafla ya Harambee katika kanisa Katoliki la Gitui.

“Maaskofu wanafaa kutoa ushauri ili kuepuka aibu inayosababishwa na vurugu kwenye makanisa yetu. Hii ni kwa sababu wao ndio wanaelewa parokia zao na wanafaa kutoa uamuzi wa mwisho,” akasema Kadinali Njue kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Akizungumza na wanahabari mjini Murang’a jana, Bw Nyoro ambaye wafuasi wake walikabiliana na wanaompinga alimlaumu Bw Kamanda kwa kujifanya mbunge wa eneo hilo na kumnyima nafasi ya kuongoza mchango wa Jumapili kanisani.

“Siwezi kuwaruhusu watu kutoka Nairobi waje na kunifunza namna ya kuendesha masuala yangu hapa Kiharu. Mimi ndiye nilichaguliwa na kama mwenyeji nina jukumu la kuwaalika wageni kuhutubu hapa,” akasema Bw Nyoro.

Vilevile, alisema kwamba anafahamu polisi wanapanga kumkamata japo akasisitiza kwamba hatishiki kwa sababu hajafanya kosa lolote.

“Najua wananitafuta kwa sababu za kisiasa na hayo yanathibitishwa na matamshi ya Bw Kamanda kwamba nitakamatwa kutokana na msimamo wangu wa kisiasa. Mimi siogopi kwa sababu sijafanya chochote kibaya,” akaongeza.

Hata hivyo, madiwani Isaac Kamote na Charles Mwangi pamoja na mwenyekiti wa Muungano wa Maaskofu wa Murang’a, Stephen Maina walimlamu Bw Nyoro kwa kusababisha ghasia za Jumapili.