SIASA NI  UTUMWA TU – KIRAITU MURUNGI

SIASA NI UTUMWA TU – KIRAITU MURUNGI

Na MWANDISHI WETU

Gavana wa Meru, Bw Kiraitu Murungi, amelazimika kuungama hadharani kuwa janga la corona limemfunua macho akabaini kuwa siasa ni utumwa ambao umewafunga watu wengi hadi wakajisahau na kukosa kujali mambo muhimu maishani mwao huku waking’ang’ania kuyalinda mamlaka.

Bw Kiraitu alisema kuwa alipokuwa akitibiwa ugonjwa huo hatari mwezi uliopita, alipata fursa ya kutafakari na kung’amua kwamba wanasiasa huwa wanaishi maisha yasiyokuwa ya kihalisia ambayo huongozwa na tamaa ya kupata na kudumisha mamlaka.

Alisema wanasiasa huwa wanaruhusu maisha yao “kuibwa” na watu wengine huku wakitawaliwa na utashi usiokoma wa pesa na mamlaka kwa kujihusisha na majukumu yasiyo na umuhimu maishani.

Akinukuu kitabu cha mwanafalsafa Seneca wa Roma kwa jina On the Shortness of Life, Bw Kiraitu alisema viongozi wa kisiasa wanajiangamiza kwa kujitwika utumwa na maisha ya kujionyesha.

“Mwanafalsafa huyo alisema kwamba ‘maisha yetu yamenaswa katika utando na dhoruba, tunarushwa huku na kule na kuzungushwa kwenye mzunguko na mawimbi yanayokinzana. Huu ndio ukweli kuhusu maisha yangu. Maisha yangu yalikuwa yameibwa na siasa na presha za kijamii,” alisema.

Alitoa mfano wa kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, ambaye licha ya kuugua corona, aliondoka nyumbani kuungana na Rais Uhuru Kenyatta kukagua miradi ya maendeleo jijini Nairobi ili kudhihirishia Wakenya kwamba handisheki yao ingali imara.

“Nilipokuwa nikisoma kitabu hicho, nilimtazama kwa huruma Bw Raila Odinga aliyekuwa mdhaifu kutokana na Covid-19 ‘akibururwa’ kutoka kitandani ili yeye na Rais waweze kuonekana pamoja wakifungua barabara Nairobi na Kajiado, kutimiza maslahi ya kisiasa, kuonyesha Wakenya kwamba handisheki ingali imara.

“Afya ya Raila haikupewa umuhimu. Siasa zilitangulizwa. Maisha yake yalikuwa yameibwa kutoka kwake. Alikuwa akiishi maisha ya kujionyesha tu. Alikuwa amenaswa katika mawimbi na dhoruba za kisiasa ambazo haziishi,” Bw Kiraitu alisema kwenye msururu wa makala yatakayochapishwa pia na Daily Nation.

Kulingana na gavana huyo, ambaye ni wakili, hatua ya Bw Odinga kutojali afya yake ni dhihirisho la jinsi siasa zimepokonya wanasiasa maisha yao.

“Maisha yetu si yetu tena. Tumetengwa mbali nasi wenyewe. Kila wakati tuko majukwaani, kujionyesha, tukitaka kutamaniwa na kupendwa na kuidhinishwa na wengine. Tunaishi maisha ya kujifanya yasiyokoma. Hatuwezi kufikiria kwa njia huru,” alisema. Bw Kiraitu anayehudumu muhula wa kwanza kama gavana, alisema alisikitika kwamba wanasiasa wamepoteza uhalisia na uhuru wao.

“Hata mawazo na sauti si zetu tena. Tunaishi maisha ya hofu kila wakati tukiwaza watu wengine wanavyofikiri kutuhusu. Kila wakati tunafuatilia hali ya siasa ili tuweze kuegemea upande unaoshinda. Muda wa kutibiwa corona ulinipa nafasi ya kutafakari kuhusu maisha yangu ya kisiasa,” aliandika.

Mwanasiasa huyo alisema kwamba siasa zilikuwa zimeteka maisha na usemi wake na uhuru wake wa kuwaza huku kila wakati akipagawa na ushindi.

“Nilikuwa nimezama katika siasa na matarajio ya wengine. Kama ningefariki kwa corona, ningefariki peke yangu. Kelele za siasa zingeendelea bila mimi. Nimefanya uamuzi wa kujipenda kuanzia sasa na kukomboa maisha yangu,” alisema.

Bw Kiraitu alisema hali ya baadaye ya siasa za Kenya haiko katika mikono ya Wakenya wa kawaida lakini iko katika mikono ya wanasiasa ambao hupanga miungano ya kisiasa kwa misingi ya makabila yao kisha wanasalitiana.

“Miungano mipya inatarajiwa katika jukwaa la siasa tunapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Kwa kuzingatia kuwa siasa za Kenya zimetawaliwa na ukabila, miungano ya kisiasa ni muhimu kwa Kenya iliyoungana, yenye amani na ustawi,” alisema na kubashiri kutakuwa na miungano mitatu mikubwa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Alisema viongozi wanaoondoka mamlakani hutaka kuwa na ushawishi kuhusu warithi wao ili walinde maslahi yao.

You can share this post!

WINNIE ONYANDO: Simu ya mwenzio sumu

Msichana akiri kubadilisha vipimo vya mimba kuokoa...