HabariSiasa

SIASA ZA 2022: Nyumba ya Jubilee inavyoyumba

October 24th, 2018 2 min read

Na GRACE GITAU

MGOGORO mpya umeibuka miongoni mwa viongozi wa Jubilee na kuibua hali inayotishia kusambaratisha chama hicho huku siasa za urithi wa urais 2022 zikizidi kutokota.

Viongozi katika chama hicho ambao ni wandani wa Rais Uhuru Kenyatta, jana waliwakemea wenzao ambao ni washirika wa Naibu Rais William Ruto, kwa kile walichodai ni mazoea ya kumdharau Rais.

Walieleza hisia zao kutokana na jinsi wenzao kutoka Rift Valley walivyoondoka ghafla katika hafla iliyoongozwa na Rais katika Kaunti ya Bomet mnamo Jumatatu.

Wabunge saba kutoka Kaunti ya Bomet, Jumatatu waliondoka katika mkutano uliosimamiwa na rais kwa hasira, wakilalamika kuwa hawakutambuliwa wala kutengewa nafasi ya kuzungumza au hata kuwapungia mkono wenyeji.

Wenzao kutoka eneo la Mlima Kenya jana walitaja kitendo hicho kama dharau kwa Rais huku wakiongeza kwamba vitendo vya kumdhalilisha rais vimekuwa vikishuhudiwa kwa muda tangu Rais alipoamua kushirikiana na Kiongozi wa ODM Raila Odinga. Walitaja pia tukio la Jumapili wakati wanasiasa wa eneo hilo walijaribu kumshinikiza Rais kumtaja mrithi wake alipokuwa Kapsabet.

Wabunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri mjini) Rigathi Gachagua( Mathira), Johnson Sakaja (Seneta, Nairobi) na Maoka Maore (Imenti Kaskazini) walidai kuna njama za kumhujumu Rais Kenyatta katika kipindi chake cha pili na cha mwisho uongozini.

“Kuna uwezekano kwamba hatua yao ilikuwa imepangwa mapema. Vitimbi walivyotuonyesha Jumapili havikuwatosha. Hakuna mtu yeyote anayefaa kuthubutu kumsawiri rais kama kiongozi asiye na mamlaka,” akasema Bw Maore.

Awali, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe, ambaye ni mmoja wa wandani wakuu wa Rais Kenyatta, aliambia wanachama kuwa hawana namna nyingine ila kuunga mkono mwafaka wa rais na Bw Odinga.

Wandani wa Bw Ruto kwa muda mrefu wamekuwa wakidai handsheki hiyo inalenga kumharibia naibu rais nafasi ya kushinda urais ifikapo 2022 ndiposa wao humtaka rais afafanue kama makubaliano yake na naibu wake bado yangali imara.

“Handsheki ipo kati ya rais na aliyekuwa waziri mkuu na tunaiunga mkono kwa sababu ni jambo jema kwa nchi. Kama Raila ataitumia kuwania urais, kuna shida gani?” akasema.

Bw Wambugu ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Naibu Rais alisema baada ya yale yaliyoshuhudiwa Jumapili, ilikuwa vyema wabunge hao kunyimwa nafasi ya kuzungumza kwa sababu ya jinsi wanavyosisitiza Rais anafaa kutangaza kwamba atamuunga Bw Ruto 2022.

Kulingana naye, kitendo cha wabunge hao kilianika wazi jinsi wanavyomchukulia Rais.

Lakini licha ya hayo yote, Bw Gachagua alisema kitendo cha Jumatatu hakikuathiri uamuzi wa viongozi wa eneo la Mlima Kenya kumuunga mkono Bw Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.