Habari za Kitaifa

Siasa za mrithi wa Ruto zinavyotishia umoja ngome yake

March 24th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

SIASA kuhusu nani atakayemrithi Rais William Ruto kama msemaji wa jamii ya Kalenjin baada ya kustaafu kwake kama rais 2032 zimechipuka tena kiongozi wa taifa akiwa katika ziara ya kikazi eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa.

Kampeni za kutwaa nafasi hiyo, zilizoanza mwaka jana, 2023, zinazosemekana kuendeshwa chini kwa chini sasa zimeleta migawanyiko miongoni mwa viongozi kutoka jamii hiyo.

Wadadisi wanaonya kuwa hali hiyo huenda itaathiri umoja haswa miongoni mwa wandani wa Rais Ruto kutoka maeneo ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa, kwa upande mmoja na Kusini mwa Bunde la Ufa, kwa upande mwingine.

Ingawa Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amelaani siasa hizo na kutaja wanaoziendeleza kama, “maadui wa ajenda za maendeleo za serikali ya Rais Ruto,” ametajwa kama mmoja wa wale wanaomezea mate wadhifa huo.

“Viongozi wa eneo hili la Bonde la Ufa wanafaa kujiepusha na siasa za ubabe za ni nani atakuwa msemaje baada ya Rais Ruto kustaafu kama Rais 2032. Bado imesalia miaka tisa kabla ya wakati huo kutimu na sasa sote tunafaa kumuunga mkono Rais ili atekeleze miradi ya maendeleo itakayobuni nafasi za ajira kwa watu wetu,”akanukuliwa akisema Jumatano akiwa Bomet kukagua miradi ya barabara kabla ya kuwasilishwa kwa Rais Ruto.

Masharti

“Baadhi ya watu wanadai kunipa masharti dhidi ya kuzuru eneo hili; hizo ni porojo ambazo hazina mashiko. Niko hapa kwa ajili ya maendeleo na sitaki nisingiziwe siasa zisizo na maana yoyote wakati kama huu,” akaongeza Bw Murkomen ambaye ni seneta wa zamani wa Elgeyo Marakwet.

Duru zinasema kuwa Gavana wa Bomet Hillary Barchok na Mbunge wa Emurua Dikkir Johanna Ng’eno wamekuwa wakimkaripia Waziri Murkomen kwa kuendesha njama za kuwahujumu katika azma yake ya kumrithi Rais Ruto kama msemaji wa kisiasa eneo hilo.

Inasemekana kuwa Bw Ng’eno anayehudumu muhula wa tatu katika bunge la kitaifa anaumezea mate wadhifa huo.

Hii ni kutokana na dhana kwamba baada ya Rais Ruto kuondoka Ikulu nafasi ya kigogo wa siasa katika jamii za Wakalenjin inafaa kuendea mtu kutoka Kusini mwa Bonde la Ufa.

Rais wa pili Hayati Daniel Moi alitoka kaunti ya Baringo iliyoko eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, huku Dkt Ruto akitoka kaunti ya Uasin Gishu iliyoko eneo lilo hilo.

“Hii ndio maana wandani wa Rais kutoka eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa ambako watu wa kabila la Wakipsigis ndio wengi zaidi wanahisi kuwa 2032 itakuwa wakati wa usemi katika siasa za jamii pana ya Wakalenjin,” anasema mchanganuzi wa kisiasa Philip Chebunet.

Kulingana na msomi huyu anayefunza katika Chuo Kikuu cha Moi, ni kutokana na imani kama hii ambapo wanasiasa wengi kutoka kusini mwa Bonde la Ufa wanakerwa na habari kwamba Bw Murkomen ni mmoja wa wale ambao wanapigiwa upato kurithi wadhifa wa msemaji wa jamii ya Wakalenjin baada ya Rais Ruto.

Kaunti jirani

“Waziri Murkomen anatoka kaunti ya Elgeyo Marakwet ambayo ni jirani ya Uasin Gishu katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa. Ndipo Bw Ng’eno na wenzake wanashikilia kuwa 2032 mwenge huo ushikiliwe na mtu kutoka eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa,” Profesa Chebunet anaeleza.

Hata hivyo, Seneta wa Nandi Samson Cherargei ambaye pia hapatani kisiasa na Bw Murkomen, amepuuzilia mbali siasa hizo za urithi wa Rais Ruto.

“Katika mila na tamaduni zetu kama Wakalenjin ni mwiko kurithi wadhifa wowote wa kijamii kutoka kwa mtu ambaye angali hai. Hii ndio maana Rais Ruto alitwaa taji hili la msemaji wa jamii ya Wakalenjin baada ya Mzee Moi kufa; sio kabla ya hao,” anasema.