Habari za Kitaifa

Siasa za Nyanza, Opiyo Wandayi akipendekezwa kumrithi Raila Odinga

March 25th, 2024 1 min read

NA RUSHDIE OUDIA

BAADHI ya washirika wa kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, kutoka eneo la Nyanza, wameanza kumpendekeza Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Opiyo Wandayi, kuwa kiongozi wao, ikiwa Bw Odinga atachaguliwa kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Kulingana na wabunge hao, lazima jamii ya Waluo iwe na usemi katika uongozi wa chama hicho, ikiwa Bw Odinga hatakuwepo.

Pia, wamesisitiza kuwa ikiwa kutakuwa na muungano wowote wa kisiasa ielekeapo 2027, jamii hiyo itachukua tu nafasi za Rais au Naibu Rais.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza mnamo Jumamosi, Machi 23, 2024 wakati wa mazishi ya Bw Tobias Lusi Oyoo (Tobby) kutoka kata ndogo ya Wang’aya 2, kata ya Kano Kusini Mashariki, kijiji cha Magare, Kaunti Ndogo ya Muhoroni.

Tobby ni kakake mbunge wa Muhoroni, Onyango K’Oyoo.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na Bw Wandayi, wabunge Samuel Atandi (Alego Usonga), Anthony Oluoch (Mathare), Dkt James Nyikal (Seme), Jared Okello (Nyando) na Dkt Joshua Oron (Kisumu ya Kati).

Bw Atandi ndiye aliyeanzisha mdahalo kuhusu urithi wa Bw Odinga, akisema kwamba hakuna mtu anayeweza kujaza pengo la kiongozi huyo, hata katika mrengo wa Azimio la Umoja.

Hata hivyo, alisema kuna viongozi wenye uwezo kutoka jamii ya Waluo, wanaoweza kuchukua uongozi kutoka kwa Bw Odinga.

“Ikiwa Raila atafanikiwa kuchaguliwa kama mwenyekiti wa AUC, lazima mmoja wetu kutoka eneo hili achukue uongozi wa ODM. Bw Opiyo Wandayi, wewe ndiye kiongozi wetu. Usiogope. Uwe mkakamavu. Enda ukabiliane na viongozi wengine na kutuongoza,” akasema Bw Atandi.