Siasa za urithi wa Ongwae zachukua mkondo wa ukoo

Siasa za urithi wa Ongwae zachukua mkondo wa ukoo

Na Wycliffe Nyaberi

MBUNGE wa Kitutu Chache Kusini Bw Richard Onyonka, amezitaka koo zingine za jamii ya Abagusii kuungana ili kukitwaa kiti cha ugavana wa Kaunti ya Kisii.

Baada ya kustaafu kwa gavana James Ongwae wa ukoo wa Abagetutu, inatabiriwa ugavana wa kaunti hiyo utamwendea mmoja wa wawaniaji kutoka koo zilizosalia za Abanyaribari, Abanchari, Ababasi, Abagirango na Abamachoge.

Hata hivyo, koo hizo zimewatoa wanasiasa wengi wanaomezea mate kiti hicho na Bw Onyonka sasa amewatahadharisha kuwa watagawanya kura zao na kuwapelekea kupoteza kiti hicho wasipoungana.

Akiongea kwenye hafla moja ya mazishi eneobunge lake, mbunge huyo alidokeza kwamba atajikita kwenye mazungumzo na wawaniaji wote wanaotaka kiti hicho ili kuunda timu itakayovuna ushindi.

“Sisi kama Abagetutu tunaelewa kwamba kuna watu wengine wanaomezea mate kiti hiki. Lakini ikiwa koo zingine zitatoa wawaniaji 33, basi jiandaeni kushindwa. Lakini kabla ya hayo nitawahusisha wawaniaji wote katika mashauriano,” Bw Onyonka akasema.

Miongoni mwa wanasiasa walioonyesha nia ya kumrithi gavana Ongwae ni mbunge wa Nyaribari Masaba Ezekiel Machogu, aliyekuwa waziri msaidizi katika serikali zilizopita Bw Omingo Magara, mbunge wa zamani wa Mugirango Kusini Bw Manson Oyongo, mwanaharakati Bi Rael Otundo, naibu gavana wa Kisii Bw Joash Maangi, waziri msaidizi katika Sekta ya Uchukuzi Bw Chris Obure na wengineo.

Wawaniaji hao wote wanatumai wataidhinishwa na Bw Ongwae ili kuimarisha nafasi yao ya kuibuka washindi.

You can share this post!

Kibarua cha IEBC kuandaa duru ya pili ya uchaguzi 2022

Lukaku pua na mdomo kurudi Chelsea