Siasa

Siasa zateka misaada

May 9th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

UHASAMA wa kisiasa kati ya Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, ulichukua mkondo wa aibu jana wakati wafuasi wao walipogeuza uhisani wa wawili hao kwa jamii kuwa ushindani.

Tangu virusi vya corona vilipoibuka nchini, kumekuwepo wahisani wengi ambao hutoa misaada kwa jamii, na viongozi wa kisiasa hawajaachwa nyuma.

Wakati huo wote, kumekuwepo maswali kuhusu hatua ambazo Dkt Ruto amechukua kusaidia jamii kwani hajakuwa akionekana hadharani kama viongozi wengine wanaojitangaza wanapotoa misaada wakati huu wa janga la corona.

Ijumaa, ilifichuliwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Dkt Ruto amekuwa akigawa chakula na vifaa vya kujikinga kutokana na corona katika mitaa ya mabanda kupitia kwa viongozi wa kidini na wanasiasa wanaomuunga mkono, ila amekuwa akifanya hivyo kimyakimya.

Lakini kilichoibua aibu ni jinsi wafuasi wa Naibu Rais walivyogeuza suala hilo la uhisani kwa maskini katika jamii kuwa ushindani kati ya vigogo hao wawili wa kisiasa.

Walirushiana cheche za maneno, kila upande ukitaka kudhihirisha ukuu na uaminifu wa mikakati ya yule anayemfuata.

“Wengine walipokuwa wakiuliza alivyokuwa akifanya na pesa alizokuwa akipatia makanisa, alikuwa anazituma kwa makanisa, misikiti na washirika wake wa kisiasa kugawa chakula katika kaunti za Nairobi, Kajiado na Kiambu,” alisema aliyekuwa mkurugenzi wa mawasiliano ya kidijitali katika Ikulu Dennis Itumbi.

Bw Itumbi, ambaye ameibuka kuwa mtetezi mkubwa wa Naibu Rais alidai kuwa kufikia Jumapili, familia 40,122 zilikuwa zimenufaika misaada kutoka kwa Dkt Ruto.

Watetezi hao wa Dkt Ruto waliwaambia wafuasi wa Bw Odinga kwamba sio lazima fujo zizuke ndipo ijulikane Dkt Ruto anasaidia maskini kwa chakula

Walikuwa wakirejelea kisa cha mtaa wa Kibra ambapo ghasia zilizuka wakati maafisa wa serikali walipokuwa wakigawa msaada wa chakula uliotolewa na Bw Odinga.

Lakini wale waliomtetea Bw Odinga walisema ni kinaya wafuasi wa Dkt Ruto kusema hataki kujionyesha ilhali wanasambaza picha za misaada wanayodai alifadhili.

“Tinga (Bw Odinga) amekuwa akisaidia watu kila mara bila kuita wanahabari; hajawahi kufadhili hashtegi ili atambuliwe. Ruto amebanwa baada ya kunyamaza kwa muda mrefu. Hana uaminifu,” akasema mtumizi wa Twitter, Abuga Makori.

Mabishano hayo yalitiwa moto saa chache baada ya mfanyabiashara wa Mombasa Hussein Shahbal kutangaza kuwa Bw Odinga aliitikia wito wake na kumpa misaada ya chakula awasilishe kwa wakazi wa Mombasa.

Wakati alipowasilisha misaada hayo kwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho jinsi inavyohitajika kikanuni, Bw Shahbal alitaka wanasiasa wakome kushindana katika mikakati ya vita dhidi ya coronavirus.

Mbunge wa kundi la ‘Tangatanga’ kutoka Mlima Kenya aliyeomba tusitaje jina lake, alithibitisha kwamba ni kweli kuna baadhi yao husambaza vyakula vilivyofadhiliwa na Naibu Rais.

Aprili 2020 Bw Odinga akionekana kumlenga Dkt Ruto, alikejeli wanasiasa ‘fulani’ kwa kunyamaza wakati Wakenya wakiteseka kwa janga la corona badala ya kuwasaidia ilhali walikuwa wakitoa mamilioni ya pesa kwenye michango makanisani kote nchini.