• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
‘Acheni domo mtupe mbinu mbadala za ukusanyaji ushuru’

‘Acheni domo mtupe mbinu mbadala za ukusanyaji ushuru’

NA RICHARD MUNGUTI

KINARA wa mawaziri Musalia Mudavadi amewataka wale wanaopinga Mswada wa Fedha wa 2023 waipendekezee serikali ya Kenya Kwanza njia mbadala za kupata fedha za kufadhili miradi ya maendeleo na kushughulikia mahitaji tele ya wananchi.

Bw Mudavadi aliwataka viongozi wa Azimio wakiongozwa na Raila Odinga wakome kabisa kutaka mswada huo wa fedha uondolewe na kufutiliwa mbali.

Kiongozi huyo alisema serikali ya Kenya Kwanza ilifanya utafiti wa kutosha kabla ya kuzindua mchakato wa mswada wa kuinua pesa za kugharimia mahitaji mbalimbali.

Bw Mudavadi alisema imebidi serikali ichukue hatua kali ambazo hazitafurahisha wananchi lakini zitakuwa za manufaa makubwa siku za usoni.

Waziri huyo alisema mswada huo ulifikiwa baada ya mashauriano makali baina ya wakuu wa asasi kadhaa za serikali miongoni mwazo Afisi ya Mwanasheria Mkuu na wataalam wa masuala ya fedha katika mamlaka ya kutoza ushuru nchini (KRA).

“Msipinge na kuyumbisha utaratibu uliowekwa na serikali wa kuinua fedha bila ya kutupatia suluhu,” Bw Mudavadi alisema huku akiongeza Azimio basi waipe serikali mawazo ya kupata pesa.

Akaongeza kusema: “Msipige kelele tu kiholela. Leteni jawabu. Lazima tutafute mbinu mwafaka za kuimarisha uchumi na kama serikali tuko na wajibu wa kuwastawisha watu wetu.”

Kinara huyu wa mawaziri alisema hayo siku moja baada ya kiongozi wa Azimio Bw Raila Odinga kumpendekezea Rais William Ruto njia atakazotumia kupata pesa bila ya kuwatoza wananchi ushuru wa ziada.

Bw Odinga alipendekeza njia 10 za kupata pesa pasi kuongeza ushuru.

Mswada huo wa fedha umepata upinzani mkali kutoka idara mbalimbali za serikali na pia kutoka kwa wadau.

Baadhi ya mapendekezo aliyotoa Odinga ni kuziba mianya yote ya ufisadi, kupunguza matumizi ya pesa katika afisi ya rais na kutambua njia ambazo huchangia kupotea kwa pesa za umma.

Odinga alisema nyongeza hizi za pesa za kodi ni njia ya kuwabebesha mzigo wananchi ambao tayari wamechoshwa na malipo ya juu ya kodi.

  • Tags

You can share this post!

MCAs wa kiume Murang’a wamulikwa kwa kuwataka wenzao wa...

Wabunge waelekezwa kwa rimoti ya Ikulu

T L