• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Azimio wasitisha maandamano baada ya Kenya Kwanza kumwondoa Keynan

Azimio wasitisha maandamano baada ya Kenya Kwanza kumwondoa Keynan

NA CHARLES WASONGA 

SIKU moja baada ya muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kuanzisha awamu ya pili ya maandamano, uongozi wake umetangaza kusitishwa kwa maandamano yaliyoratibiwa kufanyika jijini Nairobi Alhamisi, Mei 4, 2023.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Kiongozi wa Wachache Opiyo Wandayi, muungano huo umesitisha maandamano hayo kufuatia hatua ya Kenya Kwanza “kukubaliana na mojawapo ya matakwa yetu yaliyochangia kurejelewa kwa maandamano.”

“Uongozi wa Azimio ulikutana na kukubaliana kusimamisha maandamano yaliyopangiwa kufanyika kesho (Alhamisi). Hii ni baada ya Kenya Kwanza kukubaliana na mojawapo ya matakwa yetu. Badala ya kufanya maandamano, tumewaita wanachama wetu wa kamati ya mazungumzo ili wapokee maagizo mapya kuhusu namna ya kuzungumza na wawakilishi wa Kenya Kwanza,” akasema Bw Wandayi ambaye ni Mbunge wa Ugunja (ODM).

Kiongozi huyo wa wachache aliwapongeza Wakenya ambao walishiriki maandamano kutetea haki na demokrasia nchini.

Aidha, Bw Wandayi alionya kuwa Azimio haitasita kuitisha maandamano tena ikiwa vinara wake watahisi uwepo wa utovu wa moyo wa kujitolea na ukweli kutoka upande wa Kenya Kwanza.

Taarifa ya Wandayi inajiri saa chacha baada ya Kenya Kwanza kukubali kumwondoa Mbunge wa Eldas Adan Keynan kama mwanachama wa upande wao kwenye mchakato wa mazungumzo na upande wa Azimio.

Mazungumzo hayo yalisambaratika wiki jana baada ya Kenya Kwanza kushikilia kuwa haitambandua Bw Keynan kwa msingi kuwa chama cha Jubilee kilichomdhamini bungeni kimetia saini mkataba wa ushirikiano na Kenya Kwanza.

Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu alikana madai hayo na kushikilia kuwa Jubilee ingali mojawapo ya vyama tanzu katika Azimio na haijatia saini mkataba wowote wa ushirikiano na Kenya Kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Mbunge asema aliolewa akiwa kimwana bikira

Siku ya Tatu: Maiti 36 zafanyiwa uchunguzi

T L