NA CHARLES WASONGA
HATIMAYE muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya umetangaza kuwa mazungumzo ya maridhiano kati yake na Kenya Kwanza yameahirishwa hadi muda usiojulikana.
Kwenye barua aliyomwandikia mwenyekiti mwenzake, George Murugara (Mbunge wa Tharaka) mnamo Jumatano, Mei 31, 2023, Otiende Amollo (Mbunge wa Rarieda) ambaye ni mwenyekiti wa wawakilishi wa Azimio katika mazungumzo hayo, amesema wamechukua hatua hiyo baada ya Kenya Kwanza kukataa kutimiza matakwa yao.
Kulingana Dkt Amollo, Kenya Kwanza imekataa kutia saini na kuwasilisha barua ambazo ziliandikwa ziwafikie Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Hussein Marjan na mwenyekiti wa jopo la kuteua makamishna wa tume hiyo Nelson Makanda.
“Tunatambua kwamba hujajibu masuala zaidi yaliyoibuliwa katika maamuzi ya mkutano wa kundi la wabunge wa Azimio (PG) na yaliyowasilishwa kwako,” ikasema barua hiyo.
Barua ambayo Dkt Amollo amemwandikia Bw Murugara ilinakiliwa kwa vinara wa Azimio na wanachama wote 14 wa kamati hiyo ya pamoja ya mazungumzo ya maridhiano.
“Katika hali hiyo tunapendekeza kuwa hatua bora zaidi ni kuahirishwa mazungumzo hayo hadi wakati usiojulikana, kulingana na kifungu cha 36 cha mkataba wa makubaliano,” barua hiyo inasema.
Mnamo Jumanne, baada ya PG ya Azimio, viongozi wa mrengo huo walitisha kuchukua hatua ikiwa wenzao wa Kenya Kwanza hawatashughulikia matakwa yao.
Barua hiyo iliyoandikwa mnamo Mei 30, ilitumwa kwa Bw Murugara.
“Katika hali hii, tunajizuia kutoa notisi kuhusu kuvunjiliwa kwa mazungumzo chini ya kifungu cha 38 cha mkataba wa makubaliano hadi utakapojibu malalamishi yaliyotajwa hapo juu,” Dkt Amollo, ambaye ni Mbunge wa Rarieda akasema kwenye barua yake ya Mei 30.
Baada ya mkutano wa PG, kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi alisema Kenya Kwanza haijapiga hatua katika kushughulikia matakwa ya Azimio kama vile, kufanyiwa kwa marekebisho kwa Mswada wa Fedha, 2023 ili kuondoa sehemu zinazopendekeza nyongeza ya ushuru, kufunguliwa kwa mitambo ya kura ya IEBC na kupunguzwa kwa gharama ya maisha.
“Tumeipa Kenya Kwanza muda wa hadi Jumanne, usiku wa manane kushughulikia matakwa hayo ya Azimio,” akasema Bw Wandayi ambaye ni Mbunge wa Ugunja.