• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Azimio yapeleka ajenda kwa MCAs

Azimio yapeleka ajenda kwa MCAs

NA FRED KIBOR

MVUTANO unanukia kati ya madiwani na Serikali kuhusu masuala mbalimbali licha ya kwamba mazungumzo kati ya mirengo ya Rais William Ruto na Raila Odinga inalenga kukomesha joto la kisiasa nchini.

Mgawanyiko umetokea katika Muungano wa Mabunge ya Kaunti (CAF), baadhi ya wanachama wakipanga kuundwa kwa muungano utakaotetea maslahi ya madiwani pekee.

Kundi pinzani, linalooongozwa na diwani wa Kileleshwa Robert Alai, limeishutumu CAF kwa kufeli kupigania maslahi yao licha ya kwamba inafadhiliwa naa michango kutoka mabunge yote 47 ya Kaunti.

Bw Alai na wenzake wamepanga mkutano wa kitaifa jijini Nairobi Mei 3, 2023 “kuelewana na kusaka suluhu kwa matatizo yetu”. Mkutano huo utafadhiliwa na madiwani ambao wametakiwa kuchanga Sh1,000 kila mmoja.

Muungano wa CAF umelisuta kundi hilo pinzani, ukidai linaendeleza ajenda za Azimio na linataka kuchochea maandamano kwa kisingizio cha kupigania maslahi ya wanachama, ambayo muungano huo unasema umekuwa ukipigania.

Hata hivyo jana, Bw Alai alipuuzilia mbali wakosoaji wake akisema CAF imekuwa ikitumia pesa nyingi kufadhili safari za viongozi wake na kuimarisha mazingira ya utendakazi wa maspika wa mabunge ya kaunti.

“CAF haishirikishi michango ya madiwani. Maamuzi muhimu yanafanywa pasi ushirikishaji wa madiwani. Ni mafanikio yepi ambayo wameandikisha tangu kuasisiwa kwa CAF miaka minane iliyopita ikiwa wameshindwa hata kusajili muungano huo kisheria?” Bw Alai akauliza.

“Miegemeo ya vyama haifai kuingizwa katika suala hili. Kampeni inaenea kote na sio mpango unaoongozwa na madiwani wa Azimio pekee,” akasema, akidai jumla ya madiwani 1,523 wanaunga mkono juhudi zake.

“Sharti kujenga mwafaka kutoka kwa wengi wa madiwani ili kutuwezesha kuwa na asasi kama vile Tume ya Huduma za Bunge (PSC),” Bw Alai akasema.

“Kama madiwani tunahisi kuwa CAF inatubagua. Ni muungano ambao hausikizi masuala yanayotuhusu. Kuturejelea kama Azimio au Kenya Kwanza si muhimu kwa sababu tunalenga kuangazia masuala yanayoendeleza maslahi yetu,” Bw Alai akasema.

Diwani huyo alifichua kuwa madiwani kutoka kaunti za Bomet, Baringo, Nakuru, Wajir, Isiolo, Garissa, Kwale, Tana River na Mombasa wamejisajili kuhudhuria mkutano wa Mei jijini Nairobi.

Kulingana na Bw Alai muungano huo mpya utapigania nyongeza ya mishahara na marupurupu ya madiwani.

Aidha, alisema muungano huo utapigania kurejeshwa kwa marupurupu ya kuhudhuria vikao vya bunge na kuundwa kwa hazina maalum ya kufadhili miradi ya maendeleo katika ngazi za mashinani.

Madiwani hao pia wanataka marupurupu yao ya usafiri yaongezwe, uhuru wa kifedha kwa mabunge ya kaunti na walipwe pensheni kwa kuzingatia mihula waliohudumu.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi Kisumu watakiwa kuwa macho kuhusu Kipindupindu

Atumia teknolojia ya 3D kutengeneza vipuri ambavyo...

T L