• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 AM
Azimio yataka msajili wa vyama vya kisiasa atoke

Azimio yataka msajili wa vyama vya kisiasa atoke

NA CHARLES WASONGA

VINARA wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya sasa wamemtaka Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu kujiuzulu wakidai amekubali kushirikishwa katika njama ya kuhujumu demokrasia ya vyama vingi.

Wakiongozwa na kiongozi wao Raila Odinga, viongozi hao pia Jumatano waliidhinisha mabadiliko ya uongozi katika chama cha Jubilee yaliyoidhinishwa katika kongamano la kitaifa la wajumbe (NDC) la chama hicho lililofanyika Jumatatu katika uwanja wa Ngong Racecourse, Nairobi, licha ya pingamizi kutoka kwa Bi Nderitu.

“Kama Azimio, tunaunga mkono maamuzi yote yaliyofikiwa katika kongamano la kitaifa la wajumbe wa Jubilee la Jumatatu kwa sababu kongamano hili liliandaliwa kisheria na mahakama ilitoa kibali kwamba lifanyike. Kwa hivyo, Bi Nderitu hana mamlaka ya kudai mkutano huo ulikuwa haramu kwani wajibu wa afisi yake ni kutekekeza mabadiliko ya uongozi yaliyopitishwa,” akasema Bw Eugene Wamalwa aliyesoma taarifa ya Azimio kwa niaba ya wenzake.

“Kwa hivyo, tunamtaka msajili huyo wa vyama vya kisiasa kufanya mabadiliko katika uongozi wa Jubilee kulingana na maamuzi ya NDC la sivyo ajiuzulu na wadhifa huo upewe mwingine ambaye anaheshimu uhuru wa vyama vya kisiasa kujiamulia viongozi,” akaongeza mwanasiasa huyo ambaye ni kiongozi wa Chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K).

Katika mkutano huo, viongozi waasi wa Jubilee kama vile Mbunge katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega, Mbunge Maalum Sabina Chege, Naibu Katibu Mkuu Joshua Kuttuny, na mwenyekiti Nelson Dzuya walitimuliwa na nafasi zao kupewa viongozi wapya.

Aliyekuwa Katibu katika Wizara ya Usalama Saitoti Torome aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa Jubilee kuchukua mahala pa Bw Dzuya huku aliyekuwa mbunge wa Igembe Kaskazini Maoka Maore akitwa wadhifa wa naibu kiongozi wa chama hicho.

Naye Mbunge wa zamani Kigumo Jamlek Kamau aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi kuchukua nafasi ya Bw Kega huku mwanablogu Pauline Njoroge alitunukiwa wadhifa wa Naibu Katibu Mratibu.

Aidha, kongamano hilo liliongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kama kiongozi wa Jubilee, liliwataka maafisa na wabunge waasi wajiuzulu rasmi na wajiunga na muungano wa Kenya Kwanza wanaoushabikia ndani na nje ya bunge.

Lakini Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni alipowasilisha kwa afisi ya msajili mkuu wa vyama vya kisiasa majina ya maafisa hao wapya na wanachama wengine wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC), Bi Nderitu alidinda kutekelezaji mabadiliko katika uongozi wa Jubilee akidai NDC haikuandaliwa kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.

“Mkutano wa NEC ambao uliidhinisha kuitishwa kwa kongamano hilo ulihudhuriwa na wanachama sababu pekee na hivyo haikuwa halali,” Bi Nderitu akasema huku akiidhinisha hatua ya mrengo wa Bw Kega kuwafurusha chama Mbw Kioni na David Murathe, ambaye ni Naibu Mwenyekiti.

Viongozi wa Azimio pia waliiodhinisha hatua ya wawakilishi wao katika mchakato wa mazungumzo ya maridhiano kujiondoa kwa muda wa siku sababu.

“Tunaunga mkono hatua ya wenzetu kujiondoa kwa sababu Kenya Kwanza haijaonyesha nia ya kushughulikia masuala ambayo tuliwasilisha kwenye meza ya mazungumzo kama vile kupunguzwa kwa gharama ya maisha, kufunguliwa kwa Sava za IEBC na uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC kwa njia shirikishi,” akasema Bw Wamalwa.

  • Tags

You can share this post!

Mudavadi awasihi mahasla wavumilie ushuru wa juu

Shakahola: Awamu ya pili ya upasuaji maiti yaanza leo...

T L