• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
BBI: Huenda juhudi za bunge zisizae matunda

BBI: Huenda juhudi za bunge zisizae matunda

Na CHARLES WASONGA

JUHUDI za wabunge wanaoegemea mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kutumia bunge kupitisha baadhi ya mapendekezo kwenye Mswada wa BBI uliokataliwa na mahakama huenda zikagonga mwamba.

Hii ni baada ya wandani wa Naibu Rais William Ruto, wakiongozwa na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale kuomba Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kusitisha mijadala kuhusu miswada mitatu inayolenga kuvigeuza vipengele mbalimbali vya katiba.

Kwa mfano, Mswada wa Marekebisho ya Katiba inayodhaminiwa na Kamati ya Bunge Kuhusu Utekelezaji wa Katiba (CIOC), chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni, inapendekeza kumruhusu Rais kuteua baadhi ya mawaziri kutoka bungeni.

Aidha, mswada huo unapendekeza kuwa magavana pia waruhusiwe kuteua baadhi ya mawaziri kutoka mabunge ya kaunti.

Mswada unasheheni mapendekezo sawa na yale yaliyomo katika Mswada mwingine ambao umedhaminiwa na Mbunge wa Mugirango Magharibi Vincent Kemosi ambao unapendekeza kwa Rais ateue mawaziri wote miongoni mwa wabunge waliochaguliwa.

Bw Kemosi pia anapendekeza kuwa viti vya ubunge vitakavyoshindaniwa na wanawake pekee viongozwe kutoka 47 hadi 136.

Anasema dhima ya pendekezo hili ni kufanikisha hitaji la vipengele vya 47 na 81 kuhusu usawa wa kijinsia, kwamba angalau thuluthi moja ya wabunge wanafaa kutoka jinsia tofauti.

Mswada mwingine wa marekebisho ya katiba uliodhaminiwa na kamati ya CIOC unapendekeza kuwa vyama vya kisiasa viteue wagombeaji urais na wagombeaji wenzao katika Bunge la Kitaifa au Seneti kuwa wajumbe maalum.

Bw Duale ambaye ni mmoja wa wandani wakuu wa Dkt Ruto, anasema kuwa kwa kuwa mapendekezo makuu katika miswada hii mitatu yanashabihiana na yale yaliyomo kwenye mswada wa BBI uliozimwa na Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu, haipasi kujadiliwa na kuamuliwa bungeni.

“Bunge likiendelea kujadili miswada hiyo, litakuwa linakwenda kinyume na maamuzi ya Mahakama Kuu na ile ya Rufaa. Hii ni kwa sababu maamuzi yaliyotolewa na mahakama hizo yalieleza wazi kwamba marekibisho ya katiba yanayolenga kugeuza muundo wa kitengo cha utawala sharti yafanywe kupitia baraza la wawakilishi,” anasema Mbunge huyo wa Garissa Mjini.

Anaeleza kuwa kwa kupendekeza kuwa baadhi ya mawaziri wateuliwe kutoka miongoni mwa wabunge, miswada hiyo inabadili muundo wa kitengo cha utawala na hivyo kutoa nafasi kwa rais kuingilia utendakazi wa bunge.

“Hatua kama hii itafanya bunge kuwa sehemu ya kitengo cha serikali kuu na hivyo kupoteza uhuru wake. Wakenya hawafai kurejeshwa katika enzi ambapo bunge lilidhibitiwa na Ikulu ya Rais. Tutapinga vikali njama hii ya kupenyeza mapendekezo ya BBI kupitia mlango wa nyuma,” Bw Duale ambaye ni kiongozi wa zamani wa wengi aliambia safu hii kwa njia ya simu.

Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana anaunga mkono kauli ya Bw Duale akisema Bunge la Kitaifa halifai kuendelea kujadili miswada hiyo ambayo inasheheni vipengele vilivyokataliwa na mahakama.

“Ombi la Bw Duale kwa Spika Muturi kwamba asitishe mijadala kuhusu miswada hiyo lina mashiko. Bw Muturi atakuwa akipoteza muda wa bunge na rasilimali za umma endapo ataruhusu miswada hiyo kujadiliwa na kupigiwa kura,” anasema Profesa Kibwana ambaye ni mwanasheria mwenye tajiriba pana.

“Mahakama ya Rufaa ilisema waziwazi katika uamuzi wake mnamo Agosti 20, 2021 kwamba marekebisho yoyote ya Katiba yanayoathiri muundo wa utawala sharti ufanywe kupitia baraza la wawakilishi, maarufu kwa kimombo kama Constituent Assembly. Majaji sababu wa mahakama hiyo waliamua kuwa bunge halina mamlaka kama hiyo,” anaeleza huku akifananisha jaribio la bunge kufufua BBI kama “kupoteza wakati”.

Lakini Bw Kioni anapuuzilia pingamizi dhidi ya kujadiliwa kwa miswada hiyo akisema hiyo ni sawa na kuingilia mamlaka na utendakazi wa bunge.

“Ikumbukwe kwamba miswada hii ya marekebisho ya Katiba ilitayarishwa na kuwasilishwa bungeni mapema mwaka wa 2019 kabla ya kuundwa kwa mswada wa BBI. Kwa hivyo, bunge haliwezi kuzuiwa kuijadili na kuipigia kuwa kwa sababu japo ina baadhi ya vipengele vilivyoko katika BBI haikutayarishwa chini ya muktadha wa mpango huo,” anasema Mbunge huyo wa Ndaragua.

Kulingana na Bw Kioni, kipendekele cha 256 kinalipa Bunge mamlaka na uwezo wa kuifanyia Katiba marekebisho mradi mswada huo uungwe mkono na angalau wabunge 233 baada ya kujadiliwa katika awamu ya pili.

‘Endapo Bunge limeanza kushughulikia mswada wowote, mahakama au mtu yeyote hawawezi kulizuia kuendelea na mchakato huo. Endapo kuna mtu yoyote atahisi kuwa mswada fulani una dosari, sharti asubiri mswada kama huo upitishwe kisha aelekee mahakamani kuupinga,” anaeleza.

Bw Kioni anaelezea matumaini yake kwamba Spika Muturi atatupilia mbali ombi la Bw Duale na kuwaruhusu wabunge kujadili na kuamua miswada hiyo ya marekebisho.

Mbunge huyo ambaye ni mtetezi wa handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, pia anasema kuna baadhi ya mapendekezo ya BBI yenye manufaa kwa Wakenya ambayo yanafaa “kukombolewa” na wabunge.

“Mfano ni pendekeza la kuongeza mgao wa fedha kwa kaunti kutoka asilimia 15 hadi asilimia 35 ya jumla ya mapato ya kitaifa, kutengwa kwa asilimia tano ya mgao wa fedha kwa kaunti ili kufadhili maendeleo katika ngazi ya wadi, kubuniwa kwa Baraza la Vijana miongoni mwa mapendekezo mengi,” Bw Kioni anasema.

Lakini wakili Bobby Mkangi anashikilia kuwa itakuwa kazi bure kwa Bunge la Kitaifa kuendelea kuishughulikia miswada hiyo baada ya Mahakama ya Rufaa kuzima BBI.

“Suala la muundo wa kitengo cha utawala lilipewa uzito zaidi katika uamuzi wa jopo la majaji saba wa mahakama ya rufaa wakiongozwa na rais wa mahakama hiyo Daniel Musinga. Kwa hivyo, juhudi zozote za kubadili muundo wa kitengo cha utawala kinyume na walivyopendekeza majaji hao hazitafaulu,” anasema Bw Mkangi ambaye ni mmoja wa wataalamu walioandikia Katiba ya sasa.

Naibu Rais Dkt Ruto na wandani wake wamekuwa wakishabikia kuzimwa kwa BBI na mahakama wakisema ililenga kuwaongezea Wakenya mzigo kwa kubuni nyadhifa zaidi za uongozi na kurejesha Rais mwenye mamlaka makuu atakayeingilia uhuru wa Bunge na Idara ya Mahakama.

You can share this post!

Licha ya kupata makamishna 7, IEBC bado inayumba

Mzee na mwanawe wakamatwa kanisani wakivuta bangi