• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 10:55 AM
Raila awaka, Duale amchemkia

Raila awaka, Duale amchemkia

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Ulinzi Aden Duale amemshutumu kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kupendekeza kuwa mazungumzo kuhusu matakwa ya mrengo wake yanapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia mfumo wa Mpango wa Maridhiano (National Accord) ya 2007/2008.

Kwenye taarifa fupi kupitia akaunti yake ya Twitter, Bw Duale alisema Bw Odinga hafai kufananisha mzozo wa sasa na ule uliojiri nchini baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka huo.

“Bw Odinga ni mtu anayetama mamlaka kwa njia zozote zile. Anawezaje kulinganisha hali ya sasa na kipindi cha 2007/08 na kuitisha ugavi wa mamlaka kwa chini ya mfumo wa Mpango wa Kitaifa?” akasema Bw Duale.

Akiongea na wanahabari Jumanne alasiri, Bw Odinga alisema kuwa malalamishi yote ya Azimio hayawezi kushughulikiwa bungeni.

Hii ni tofauti na kauli ya Rais William Ruto kwamba matakwa yote ya Azimio, yaliyochochea maandamano, yanaweza kushughulikiwa kupitia maelewano bungeni.

“Ni msimamo wetu kwamba masuala yetu yote hayawezi kushughulikiwa bungeni. Masuala kama gharama ya maisha, ukaguzi wa sava za kupokea matokeo ya uchaguzi wa urais, mabadilik na uteuzi wa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na uzingative wa misingi ya demokrasia ya vyama vingi.

“Tunapendekeza kwamba masuala haya yashughulikiwe nje ya bunge kwa mfumo wa Mpango wa Maridhiano kama ya mwaka wa 2007/08,” Bw Odinga akawaambia wanahabari katika kituo cha SKM Command Centre, mtaani Karen.

Bw Odinga alipendekeza kuwa mazungumzo hayo yaendeshwe na kundi lenye uwakilishi kutoka ndani na nje ya bunge, na ambalo wanachama wake watateuliwa kutoka mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio.

Mpango wa Maridhiano, ambalo Bw Odinga alikuwa akirejelea ni ule wa mwaka wa 2008 ambao ulifanikisha mwafaka kati yake na Hayati Rais Mwai Kibaki.

Mpango huo ambao ulisimamiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Koffi Annan na ambao upendekeza ugavi wa mamlaka kati ya mirengo mbili hasimu katika mzozo huo uliochangiwa na utata kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Ni kupitia mwa mpango huo ambapo Bw Odinga alipata nafasi ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Muungano Mkuu.

Jumanne, Bw Odinga aliweka wazi kwamba matakwa yao manne sharti yatimizwe na serikali.

Hayo ni; kupunguzwa kwa gharama ya maisha, ukaguzi wa sava za IEBC (zoezi hilo liendeshwe na wataalamu, uteuzi wa makamishna wa IEBC kwa njia inayoshirikisha wadau wote na uzingativu wa msingi ya demokrasia ya vyama vingi bungeni.

  • Tags

You can share this post!

Mshtakiwa atishia kutoa nguo kortini athibitishe anaugua...

CJ Koome kuteua majaji watakaoamua kesi kupinga uteuzi wa...

T L