• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
Fanya fujo uone, Ruto aonya Raila

Fanya fujo uone, Ruto aonya Raila

NA JUMA NAMLOLA

NAIBU Rais William Ruto ametoa onyo kali kwa mgombeaji urais wa chama cha Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga kwamba, atakiona cha mtema kuni akileta fujo baada ya kumshinda.

Dkt Ruto anasema yeye si mtu wa kuchezewa kama Rais Uhuru Kenyatta, na kwamba iwapo Bw Odinga atajaribu kujiapisha baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, atajua kuwa serikali ina mkono mrefu.

Kwenye mazungumzo yaliyoonekana kumtahadharisha Bw Odinga, Dkt Ruto alisema ana uhakika wa kushinda, na kama kinara huyo wa chama cha ODM anajipenda, asithubutu kuitisha maandamano au kupinga matokeo ya uchaguzi.

“Na nimemwambia, kwa sababu si mlisikia Rais akisema, ati huyu mtu alikuwa anataka kuleta kisirani. Mlisikia Uhuru akisema huyu mtu alitaka kumwaga damu sijui nini 2017. Mimi nimemwambia bwana Kitendawili, Mimi si Uhuru Kenyatta utaniletea. Mimi nitaangalia wewe macho kwa macho,” akasema alipohutubu kwenye mkutano wa kujipigia debe eneo la Karuri, Kiambu.

Dkt Ruto anadai kuwa Bw Odinga anajiweka mbele kwenye kura za maoni, ili akishindwa akatae matokeo.

“Safari hii, hakuna kujiapisha. Hakuna kutupa mawe. Hakuna kupanga maandamano. Hakuna mambo ya eeh, Tibiim, Tialala. Tukimalizana na wewe, unaenda nyumbani polepole. Na ukihitaji usaidizi, tuko na wilbaro. Ile ya mguu kubwa. Tuweke Kitendawili, buga buga buga mpaka Bondo,” akaeleza.

Baada ya kupoteza kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017, Bw Odinga na wafuasi wake wa muungano wa National Super Alliance (NASA), walikusanyika katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi Januari 30, 2018 na kumuapisha kuwa ‘Rais wa Wananchi’.

Kitendo hicho kilitajwa kuwa cha uhaini na kuna watu katika serikali ya Jubilee waliotaka Bw Odinga anyongwe. Lakini baadaye, Rais Kenyatta alisalimiana naye katika kile kinachofahamika hasa kama handisheki.

Lakini Dkt Ruto anasema endapo atatangazwa mshindi, hatakubali kitendo cha aina hiyo, wala malalamishi ya Bw Odinga na wafuasi wake wa Azimio kukataa matokeo au kulalama iwapo watahisi kuwepo udanganyifu.

“Si mumeona huyu jamaa ameanza ile kazi yake ya kawaida? Anasema ako na shida na Chebukati. Amesema tena ako na shida na rejista. Tayari imebainika wazi ya kwamba, sisi tutashinda huu uchaguzi. Wale tunashindana na wao, kwa sababu wamekwama, sasa wanazungusha kura za maoni. Tarehe tisa mwezi wa nane, watakutana na wananchi kwa debe. Hakutakuwa na sinema, hakutakuwa na kura na maoni. Wakenya wenyewe wataamua.”

Dkt Ruto amekuwa akikataa kura za maoni za kampuni za Infotrak na Trends and Insight for Africa (TIFA), ambazo zimemuonyesha Bw Odinga akiwa mbele yake.

Matokeo ya kura ya maoni ya TIFA wiki jana yalionyesha kuwa, kama Uchaguzi Mkuu ungefanyika, asilimia 42 wangempigia Bw Odinga huku 39 walimpa Dkt Ruto.

Nayo ya Infotrak inamuonyesha Bw Odinga akiwa mbele kwa asilimia 43 dhidi ya asilimia 37 ya Dkt Ruto.

Lakini naibu rais na wafuasi wake katika Kenya Kwanza, wanasema hizo kura za maoni haziwatishi, kwa kuwa Bw Odinga amekuwa akiwekwa mbele kila mwaka wa uchaguzi, na mwishowe huishia kushindwa na kuzua fujo.

“Huyu mtu kila tukifika uchaguzi, anaenda anatengeneza kura za maoni bandia. Alikuwa mbele ya Mwai Kibaki katika kura za maoni. Akawa mbele ya Uhuru Kenyatta katika kura za maoni. Sasa anasema ako mbele yangu kwa kura ya maoni. Lakini alienda nyumbani, hakuenda?” akauliza.

You can share this post!

Rai Wakenya wasiwachague wafisadi Agosti

LISHE: Faida za kusikusi

T L