• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Gachagua apinga handisheki akisaka ubabe Mlima Kenya

Gachagua apinga handisheki akisaka ubabe Mlima Kenya

MWANGI MUIRURI Na GEORGE MUNENE

NAIBU wa Rais Bw Rigathi Gachagua amezidisha kampeni zake za kusaka ubabe wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.

Bw Gachagua katika siku za hivi karibuni amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara katika Kaunti za Murang’a, Kirinyaga, Nyeri, Laikipia, Nyandarua na Kiambu huku akijipigia debe kwa wakazi kwa kushambulia Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kwa madai kwamba, anahujumu biashara za wakazi wa eneo la Mlima Kenya.

Naibu wa Rais pia amekuwa akitumia ziara zake katika eneo la Mlima Kenya kushambulia kinara wa Azimio Raila Odinga kwa kuongoza maandamano dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza na ‘kuharibu biashara ya watu wa Mlima Kenya’.

Jana Jumatano, Bw Gachagua alikuwa katika Kaunti ya Embu ambapo alishambulia Bw Odinga na kumtaka kusahau handisheki baina yake na Rais William Ruto.

“Rais hayuko tayari kukutana na Bw Odinga kujadili jinsi ya kugawana serikali,” Bw Gachagua alisema alipozuru kaunti ya Embu.

“Yule mzee wa maandamano amekuwa na kupiga kelele, tumekataa uharibifu zaidi wa mali,” aliongeza.

Bw Gachagua alisisitiza kuwa serikali iko tayari kulinda mali ya Wakenya.

Akizungumza baada ya kukagua soko la Embu, Bw Gachagua alisisitiza kuwa Dkt Ruto alishinda uchaguzi wa urais kwa njia ya haki na ataendelea kuhudumia Wakenya wote bila ubaguzi.

Mnamo Jumatano, Bw Gachagua alikuwa katika Kaunti ya Kirinyaga ambapo alizidisha pingamizi zake kuhusu handisheki kati ya Rais Ruto na kinara wa Azimio Bw Raila Odinga akisema kuwa Mlima Kenya hautathubutu kuunga mkono maelewano ya aina hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Kamanda wa GSU kuapishwa Naibu Inspekta Jenerali

Kindiki atolewa jasho Bungeni

T L