• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 11:55 AM
Hofu kuu ya Ruto ni kuibiwa kura 2022

Hofu kuu ya Ruto ni kuibiwa kura 2022

NA BENSON MATHEKA

Kila dalili zinaonyesha kuwa Naibu Rais William Ruto anahofia kwamba ataibiwa kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Hii ni kwa sababu amekuwa akilaumu mawaziri wanaosimamia idara za usalama na teknolojia kwa kuhusishwa katika shughuli za kuandaa uchaguzi mkuu ujao.

Dkt Ruto na washirika wake wanalaumu mawaziri Fred Matiang’i ( Usalama wa Ndani) na Joe Mucheru ( Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Ubunifu na Masuala ya Vijana) kwa kupanga njama ya kumpokonya ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wadadisi wa masuala ya siasa na uchaguzi wanasema kwamba Kauli zake na washirika wake katika chama cha United Democratic Alliance (UDA) za kukashifu mkutano wa mawaziri hao wawili na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zinaonyesha kwamba anahofia kumnyimwa ushindi katika kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Tayari chama cha UDA kimeandikia barua IEBC kikitaka mawaziri hao wawili kuondolewa katika kamati inayosaidia tume kufanikisha uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Mawaziri hao wawili na Jaji Mkuu Martha Koome walikuwa miongoni mwa wadau waliokutana na IEBC Jumatatu wiki mbili zilizopita kujadili maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.

Tangu mkutano huo, Dkt Ruto na washirika wake wamekuwa wakidai kuna njama ya kumuibia kura.

Kulingana na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, ingawa Dkt Matiang’i na Bw Joe Mucheru wanasimamia wizara zinazohusiana moja kwa moja na uchaguzi mkuu, wametangaza wazi kuwa wanamuunga kiongozi wa chama cha ODM Raila, mpinzani mkuu wa Dkt Ruto na wanatilia shaka mkutano wao na IEBC.

TEKNOLOJIA

“Dkt Matiang’i anasimamia polisi ambao wanahusika na usalama wakati wa kampeni na uchaguzi, naye Bw Mucheru anasimamia tekinolojia ambayo ni muhimu kwenye uchaguzi na kupeperusha na kujumuisha matokeo ya kura. Tumeona wakiidhinisha hadharani mpinzani wetu mkuu na kwa hivyo hakuna imani nao. Wanafaa kujiuzulu,” alisema Bw Nyoro.

Akiwa Nyamira wiki tatu zilizopita, Dkt Matiang’i alisema atamuunga Bw Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya kwa kuwa ndiye chaguo la mkubwa wake Rais Kenyatta. Bw Mucheru naye amewahi kunukuliwa akikosoa vikali kampeni ya kuinua uchumi ya Dkt Ruto.

Bw Nyoro anasema kwamba Wizara ya Bw Mucheru inasimamia Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) inayoshirikiana na IEBC kwenye uchaguzi.

“Hatuwezi kuruhusu watu ambao ni mawaziri katika wizara muhimu katika wakati kama huu kuwa na mapendeleo,” aliongeza Bw Nyoro.

Dkt Ruto ambaye ametengwa serikalini kufuatia uhusiano wake baridi na Rais Kenyatta amekuwa akidai kwamba watu wenye ushawishi ndani na nje ya serikali wamekuwa na njama ya kumzuia kuingia ikulu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Ingawa amekuwa akidai kuwa ni raia watakaoamua atakayewaongoza, kauli za hivi punde za washirika wake zinaonyesha kwamba anahofia kuwa atapokonywa ushindi.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba hofu ya Dkt Ruto inatokana na kukosa habari za kijasusi alizokuwa akipata kabla ya kutofautiana na Rais Kenyatta.

“ Hii ndiyo sababu analalamika hata kwa mambo ambayo anajua ni ya kawaida kama mawaziri wa usalama wa ndani na Tekinolojia kusaidia IEBC kushirikiana na IEBC kuandaa uchaguzi. Kusema kweli hofu yake haina msingi na inanuiwa kuchochea wafuasi wake mapema akishindwa,” asema mchanganuzi wa siasa Peter Kinama.

Anasema Dkt Ruto hakuibua masuala kama hayo mawaziri hao waliposhirikiana na IEBC katika uchaguzi mkuu wa 2017 aliyokuwa mgombea mwenza wa Rais Uhuru Kenyatta.

“Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017 alikuwa akimtetea Bw Matiang’i kutoka lawama za viongozi wa upinzani.

Hii ni kwa sababu alikuwa akipata ripoti za ujasusi kwa vile hakuwa ametengwa serikalini,” asema mchanganuzi wa siasa Dominic Wekesa.

Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa UDA, Veronica Maina alisisitiza kuwa Dkt Matiang’i na Bw Mucheru hawafai kuwa kwenye kamati ya kufanikisha uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Kulingana naye, UDA kinashikilia kuwa wawili hao wanafaa kuhamishwa au kujiuzulu.

You can share this post!

Mke aliyetemwa na mumewe achoma nyumba

Meza wembe, Kibicho amwambia Ruto

T L