• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
JAMVI: Huyu atakayembwaga Ruto Mlimani ni nani?

JAMVI: Huyu atakayembwaga Ruto Mlimani ni nani?

Na BENSON MATHEKA

MABWANYENYE kutoka Mlima Kenya wanaodadisi wagombeaji urais wanakabiliwa na kibarua kigumu kumuidhinisha atakayeweza kumbwaga Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Dkt Ruto amepenya eneo la Mlima Kenya bila baraka za Rais Uhuru Kenyatta ambaye amekuwa akimlaumu kwa kumdharau na kumhujumu.

Mabwanyenye hao wenye ushawishi mkubwa wanasema kwamba wametumwa na Rais Kenyatta kuwahoji wagombeaji urais ili kumshauri anyeafaa kutetea na kulinda maslahi ya wakazi wa eneo la Mlima Kenya.

Wamekutana na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga waliyemmiminia sifa kwa kumsaidia Rais Kenyatta kwenye muhula wake wa pili uongozini wakisema kuna watu waliotaka kumhujumu.

Hii imechukuliwa na wengi kuwa waziri mkuu huyo wa zamani ndiye chaguo la matajiri hao kwa kuwa anaungwa na Rais Kenyatta.

Mnamo Alhamisi, walikutana na vinara wa muungano wa One Kenya Alliance Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi ( ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu) kwa mazungumzo kuhusu ajenda zao kwa eneo la Mlima Kenya.

Duru zinasema baada ya mikutano hiyo miwili iliyofanyika katika hoteli ya Safari Park, Nairobi, kibarua cha matajiri hao ni kushawishi viongozi hao wa upinzani kuunga mmoja wao.

Bw Odinga hajatangaza azma yake ya kugombea urais japo amekuwa akiendeleza kampeni ya kujipigia debe chini ya kauli mbiu ya Azimio la Umoja na anaungwa mkono na Rais Kenyatta.

Katika OKA, Bw Mudavadi, Bw Musyoka na Bw Moi wametangaza kuwa watagombea urais na tayari wamekabidhiwa tiketi na vyama vyao huku washirika wao wakishikilia kuwa ni lazima majina yao yawe kwenye debe kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wadadisi wa siasa wanasema Dkt Ruto ambaye amepuuza mikutano ya matajiri hao na wapinzani wake, anafurahia kibarua kigumu ambacho kinawakabili mabwanyenye hao kutafuta mgombeaji mmoja wa kumenyana naye.

“Kwanza, itabidi wafanyabiashara hao washawishi vinara wa OKA kuunga mmoja wao ili waamue iwapo atakuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga. Japo wanasisitiza kwamba hawajaamua chaguo lao, ni wazi kama mchana kwamba chaguo la Rais Kenyatta wanayekiri aliwatuma ni Bw Odinga,” asema mchanganuzi wa siasa Betty Shayo.

Anasema jambo jingine linalowafanya wafanyabiashara hao kujikuna kichwa, ni kitakachofanyika wakiteua mgombea mwenza wa Bw Odinga mgombeaji urais mwingine kutoka eneo la Mlima Kenya.

“Kuna wasiwasi kwamba iwapo watateua mgombea mwenza wa Bw Odinga au wa mgombea urais wa muungano wa OKA kutoka eneo lao Mlima Kenya uasi utatokea na baadhi ya viongozi kuungana na Dkt Ruto,” asema Shayo.

Naibu Rais William Ruto (kulia) akiwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika hafla ya awali. Picha/ Maktaba

Hata kabla ya kuteua mgombeaji urais na mgombea mwenza, aeleza mchanganuzi wa siasa Peter Kamunya, matajiri hao wanakabiliwa na kibarua sawa na kilichomkabili Rais Kenyatta mwenyewe alipojaribu kupatanisha Bw Odinga na vinara wa OKA.

Katika mkutano wa Alhamisi, vinara wa OKA waliwaambia wafanyabiashara hao kwamba juhudi za kuwashinikiza kuunga Bw Odinga zitagonga mwamba.

Kulingana na aliyekuwa mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo ambaye aliandamana na vinara hao katika mkutano huo, itakuwa kuharibu wakati kuwataka kuunga mgombeaji wasiyetaka.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Mount Kenya Foundation Bw Peter Munga na Naibu Wake Titus Ibui walisema kwamba watatoa uamuzi katika kongamano la tatu la Limuru litakalowaleta pamoja viongozi wa kisiasa, kibiashara, kijamii, kidini na vijana.

Baadhi ya wanasiasa na wadadisi wanasema kwamba vinara wa OKA wanafaa kuungana na Bw Odinga kumzuia Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Hofu ya wanamikakati wa Rais Kenyatta, wakiwemo wafanyabiashara hao ni kuwa iwapo upinzani utagawanyika itakuwa vigumu kumshinda Dkt Ruto.

Kinachowafanya wajikune kichwa ni kuwa hakuna viti vikubwa vya kugawia vinara wote baada ya kuzimwa kwa mchakato wa kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao ulianzishwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Inasemekana kuwa japo wangetaka eneo lao kuwakilishwa katika serikali kuu, chini ya katiba ya sasa, kuteua mgombea urais kutoka Mlima Kenya kunaweza kusambaratisha mipango yao ya kumzuia Dkt Ruto.

Naibu Rais ameashiria kuwa atateua mgombea mwenza kutoka Mlima Kenya na ikizingatiwa ufuasi wake eneo hilo umeongezeka pakubwa, kutoungana kwa upinzani kunaweza kuvuruga mipango ya kumzuia kuingia Ikulu.

“Itabidi mabwanyenye hao kuunganisha vinara wa OKA na Bw Odinga, wafanye kampeni ya hali ya juu mashinani kubomoa umaarufu wa Dkt Ruto ili kujenga imani ya wakazi kwa Bw Odinga iwapo watamtawaza kuwa chaguo la mrithi wa Rais Kenyatta,” asema Shayo.

“Iwapo wataamua kuunga mgombeaji mwingine, jambo ambalo ni finyu sana kwa sasa, itabidi wamshawishi Bw Odinga na ngome zake kumuunga mkono,” aongeza.

You can share this post!

TAHARIRI: Shule zisiwafukuze wanafunzi kiholela

Unywaji pombe unachangia matatizo ya akili – Nacada