• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Jubilee haitambembeleza Kuria, atatimuliwa chamani – Murathe

Jubilee haitambembeleza Kuria, atatimuliwa chamani – Murathe

Na SAMMY WAWERU

CHAMA tawala cha Jubilee (JP) kimetishia kumtimua mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kwa kile kimedai ni “kukiuka sheria za chama”.

Naibu mwenyekiti wa JP David Murathe amesema Bw Kuria ameenda kinyume cha sheria za chama, kwa kumpigia debe mwaniaji wa PEP, George Koimburi kufuatia uchaguzi mdogo wa eneobunge la Juja unaotarajiwa kufanyika.

“Kisa cha Moses Kuria ni wazi amekiuka kanuni za chama kwa kumfanyia kampeni mgombea ambaye si wa chama kilichomuingiza bungeni,” akasema Bw Murathe.

Kuria ndiye kiongozi wa PEP, chama ambacho kimezua ushindani mkali dhidi ya mgombea wa Jubilee, Susan Njeri Waititu katika uchaguzi wa Juja.

“Chama hakina budi ila kumfurusha,” Murage akaonya.

Kiti cha ubunge Juja kilisalia wazi kufuatia kifo cha Francis Waititu mnamo Machi 2021.

Bi Njeri ndiye mjane wa mbunge huyo, ambaye anamezea mate wadhifa ulioachwa wazi na mume wake.

Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi (NMC) Jubilee, Jumatano iliamuru kamati ya nidhamu kuanza mikakati ya kumtimua Bw Kuria pamoja na wabunge kadha maalum kwa kukiuka sheria za chama.

You can share this post!

WhatsApp kuanza kutekeleza masharti mapya Jumamosi

Mtihani mgumu unaosubiri Mkenya Onyango kuingiza wanaraga...