• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Kalonzo hasaidiki, adai Rais

Kalonzo hasaidiki, adai Rais

NA MARY WANGARI

RAIS William Ruto amefichua jinsi alivyojaribu bila mafanikio kumwokoa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kutokana na mahangaiko yake kisiasa kama kinara mwenza wa muungano wa Azimio.

Akizungumza  Jumapili katika Kaunti ya Machakos, Kiongozi wa Taifa aliwaeleza wakazi wa eneo hilo jinsi alivyojitolea kutimiza ahadi yake ya kumtafuta Bw Kalonzo na kumjumuisha katika serikali yake ya UDA baada ya kura mwaka 2022.

Rais Ruto alifichua jinsi walivyoshiriki kikao na Bw Musyoka na kumshawishi wafanye kazi pamoja ila akakataa na kuamua kusalia katika upinzani pamoja na kinara wa Azimio Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua.

Dkt Ruto alisema alichukua hatua hiyo ya kumtafuta kinara wa Wiper ili kutimiza ahadi aliyoipa jamii ya Wakamba alipokuwa akisaka kura kwenye kinyang’anyiro cha ikulu kilichofanyika Agosti 9.

“Wakati nilikuja kuomba kura nilisimama hapa, nikasimama Kitui, nikasimama Wote, nikasimama Mwingi. Na mimi niliwaahidi kuwa mkinipa nafasi ya kuongoza taifa letu sitawaacha watu wa Ukambani nyuma,” alisema Rais Ruto.

“Hata niliwaambia nikipata ushindi nitatafuta yule rafiki yangu Kalonzo kwa sababu amesumbuliwa sana na wale jamaa. Na mimi sitaki kuwa mtu mwongo. Niliposhinda uchaguzi, vile niliwaeleza, nilimtafuta na nikaketi chini naye. Nikamwambia, si unajua sasa mimi nimeshinda uchaguzi. Sasa wewe kuja hapa tuunde serikali. Kuna kiti cha Spika na kuna kingine, tafuta Wakamba tuwaingize twende mbele,” alisema.

“Kwa sababu sitaki mnilaumu baadaye mkasema mbona William Ruto alituambia akishinda atatafuta Kalonzo waongee kwa sababu ameteswa sana na wale watu. Mimi nimetimiza wajibu wangu. Yeye mwenyewe akaniambia anataka kuendelea kuwa upinzani. Sasa ningefanya nini?”

Licha ya Bw Kalonzo kukataa kushirikiana na serikali ya UDA, Rais Ruto alisisitiza kuwa yupo tayari kushirikiana na viongozi wengine katika eneo la Ukambani kwa manufaa ya eneo hilo na Wakenya wote.

“Nataka mnieleze nimefanya makosa? Si ni vizuri tuungane kama viongozi ili kupeleka Kenya mbele na pia nipate nafasi nipange mambo ya maendeleo ya taifa letu na Wakenya vilevile!”

Rais aliyekuwa ameandamana na viongozi kadhaa wa UDA akiwemo Naibu Rais Rigathi Gachagua alitangaza mikakati kadhaa ya kufanikisha maendeleo Ukambani hususan kuhusu tatizo la maji na kilimo.

Mikakati hiyo ambayo yamkini ni ya kuvutia jamii ya Wakamba kuunga mkono serikali ya Dkt Ruto ni pamoja na mradi wa Sh500 milioni unaodhamiriwa kukomesha tatizo sugu la ukosefu wa maji katika maeneo ya Machakos, Yatta na Kitui.

Mpango wa kuanzisha Kituo Kikuu cha Viwanda vya Bidhaa za Kilimo katika Kaunti ya Machakos utakaogharimu Sh250 milioni kupitia ushirikiano kati ya serikali kuu na serikali ya kaunti.

Aidha, Rais alitangaza mipango ya kupanua ujenzi wa nyumba za bei nafuu hadi nyumba 5,000 kutoka 2,000 hatua ambayo alisema itawapa ajira vijana wapatao 7,000 kama vile waashi, maseremala, mafundi wa stima na kazi nyinginezo.

  • Tags

You can share this post!

Atumia teknolojia ya 3D kutengeneza vipuri ambavyo...

UEFA: Real Madrid wala mori ya kumaliza kazi dhidi ya...

T L