• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
KANU yamteua Gideon Moi kuwania urais 2022

KANU yamteua Gideon Moi kuwania urais 2022

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa chama cha KANU Bw Gideon Moi ameteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao, 2022.

Bw Moi ambaye pia ni seneta wa Baringo alipewa tiketi hiyo Alhamisi katika kongamano la KANU, lililofanyika Ukumbi wa Bomas, jijini Nairobi.

Mara ya mwisho KANU kuwa mamlakani ilikuwa mwaka wa 2002, Rais Daniel Arap Moi, ambaye kwa sasa ni marehemu, alipostaafu, Rais (mstaafu) Mwai Kibaki akimrithi kama rais.

“KANU imekuwa likizo tangu 2002,” Bw Moi akasema, akihutubia wajumbe waliokongamana.

Aidha, seneta huyo alisema chama chake kimekuwa kikishirikiana na vyama vingine kuendeleza miradi ya maendeleo nchini.

“Kipindi cha muda ambao tumekuwa nje ya serikali, tumekuwa tukishirikiana na vyama mbalimbali na kutathmini mipango ya siku za usoni.

“Muda wa kurejea uongozini umewadia, si mwingine ila ni sasa hivi (akimaanisha kupeperusha bendera ya KANU kuwania kiti cha urais,” akafafanua.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetangula (Ford-Kenya), na Isaack Ruto (Chama Cha Mashinani) ni kati ya wageni mashuhuri waliohudhuria hafla hiyo.

Akiahidi kwamba hivi karibuni atazindua sera zake kuwania urais 2022, Bw Moi alisema mojawapo ya ajenda atakazotilia maanani ni vita dhidi ya ufisadi.

Seneta huyo ni miongoni mwa vinara wa Okoa Kenya Alliance (OKA), muungano unaojumuisha Mabw Kalonzo, Musalia na Wetangula.

You can share this post!

Wizara ya Kilimo inavyoshirikisha vijana na kuwapa motisha...

Kanini Kega abadili kauli ya kumuunga Raila 2022, asema...