• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
Kenya Kwanza yarai Azimio kurejelea mazungumzo

Kenya Kwanza yarai Azimio kurejelea mazungumzo

NA CHARLES WASONGA

WAWAKILISHI wa Kenya Kwanza katika kamati ya mazungumzo ya maridhiano wamewasuta wenzao wa Azimio kwa kujiondoa kwa muda wakilalamikia kutoshughulikiwa kwa matakwa yao kadhaa.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao George Murugara, wabunge hao wamesema Alhamisi kuwa ilikuwa mapema kwa wenzao wa Azimio kuchukua hatua hiyo bila kufuata taratibu zote za kusuluhisha tofauti baina yao.

“Ilikuwa ni mapema kwa wenzetu wa Azimio kuchukua hatua kama hiyo kwa msingi wa sehemu ya 27 ya makubaliano ya kuendesha shughuli za kamati. Wenzetu walisahau kwamba kuna sehemu ya 34 inayosema kuwa ikiwa tutakosa kukubaliana, wenyeviti wenza wanaweza kuketi na kujadili masuala hayo na kukubaliana. Waliruka sehemu hii,” amesema Bw Murugara kwenye kikao na wanahabari katika Majengo ya Bunge.

Mbunge huyo wa Tharaka ameahidi kumwalika mwenyekiti wa upande wa Azimio Otiende Amollo kwa mkutano Jumatatu saa nane na nusu alasiri “kuona ikiwa tutapatana tena.”

“Hii ni kwa sababu sisi wawakilishi wa upande wa Kenya Kwanza katika kamati hii tuko tayari kurejelea mazungumzo haraka iwezekanavyo,” ameongeza Bw Murugara.

Wawakilishi wa Kenya Kwanza katika kamati ya mazungumzo ya maridhiano wakitoa taarifa kwa wanahabari katika Majengo ya Bunge, Nairobi mnamo Mei 25, 2023. PICHA | CHARLES WASONGA

Mnamo Jumatano vinara wa Azimio walitoa makataa ya siku sita kwa mrengo wa Rais William Ruto wa Kenya Kwanza wakitaka malalamishi yao yashughulikiwe kwanza ikiwemo kutoingiliwa kwa chama cha Jubilee.

Viongozi hao wa upinzani walitoa makataa hayo baada ya kufanya mkutano na Otiende na wenzake wanaowakilisha Azimio kwenye kamati hiyo ya pamoja ya watu 14.

Kwenye taarifa iliyosomwa na kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa, walilaani Kenya Kwanza wakisema mrengo huo haujaonyesha moyo wa kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na Azimio kama vile kupanda kwa gharama ya maisha, ukaguzi wa mitambo ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), uteuzi wa makamishna wa tume hiyo kwa njia jumuishi na kukomesha mtindo wa kuingilia vyama tanzu katika Azimio.

  • Tags

You can share this post!

Mkongwe kutembea kilomita 300 kuadhimisha Madaraka Dei 2023...

Kafyu katika eneo pana la Chakama yaongezwa kwa siku 30...

T L