• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Kiazi moto kwenye mjadala wa Bomas

Kiazi moto kwenye mjadala wa Bomas

BENSON MATHEKA Na WANDERI KAMAU

MIRENGO ya Azimio na Kenya Kwanza ingali inavutana kuhusu baadhi ya ajenda za mazungumzo ya pande mbili yanayotarajiwa kutatua mzozo wa kisiasa ambao umedumu nchini kwa mwaka mmoja sasa.

Pande zote zimeteua kamati za kiufundi kukubaliana kuhusu ajenda za kujadiliwa lakini kufikia jana, hazikuwa zimepiga hatua.

“Kama mnavyojua pande zote zilikuwa na ajenda zake na punde tu muafaka utakapoafikiwa na kamati za kiufundi tutaweza kusonga mbele,” kiongozi wa mrengo wa Azimio katika mazungumzo hayo Kalonzo Musyoka alisema Jumatatu.

Mwenzake wa Kenya Kwanza Kimani Ichung’wah alisema japo walikuwa wamewaeleza wanachama wao katika kundi hilo kuhusu mazungumzo, wanataka kuwaeleza zaidi matokeo wanayotarajia.

“Tunataka kukamilisha shughuli hii kwa muda mfupi iwezekanavyo na kuifanya kwa misingi ya kikatiba,” akasema Bw Ichung’wah.

Masuala ya Azimio ambayo Kenya Kwanza imekuwa ikikataa ni gharama ya maisha, kukaguliwa kwa sava za uchaguzi wa urais wa mwaka wa 2022 na ukatili wa polisi.

“Masuala yetu hayajabadilika, ni lazima tujadili gharama ya maisha inayoathiri watu wetu, kukaguliwa kwa matokeo ya kura ya urais ili kurekebisha dosari katika uchaguzi, hatua za kuzuia kuingilia vyama vya kisiasa na ukatili wa polisi,” akasema kiongozi wa Azimio Raila Odinga kabla ya pande zote kukutana katika Bomas of Kenya wiki jana.

Kenya Kwanza chini ya Rais William Ruto nayo imeorodhesha kubuniwa kwa wadhifa wa kiongozi rasmi wa upinzani bungeni, kuwekwa kwa hazina ya maeneo bunge katika Katiba, kutambuliwa kwa wadhifa wa mkuu wa mwaziri na kutekelezwa kwa kanuni ya usawa wa jinsia.

IEBC

Suala la pekee ambalo halina ubishi katika mazungumzo hayo ni kuundwa upya kwa Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC).

Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot, wabunge Hassan Omar (Bunge la Afrika Mashariki-EALA), Catherine Wambilianga (Bungoma) na Gavana Cecily Mbarire (Embu) wanawakilisha Kenya Kwanza chini ya Bw Ichung’wah.

Azimio inawakilishwa na Bw Musyoka (kiongozi wa ujumbe), Seneta Okong’o Omogeni (Nyamira), Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi, mbunge Amina Mnyazi (Malindi) na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa.

Kauli za Kalonzo na Ichungwah zinaashiria mvutano kati ya pande zote mbili zinazoshiriki kwenye Mazungumzo hayo ya Maridhiano huku duru zikieleza kuwa hazijakubaliana kuhusu masuala kadhaa tata.

Duru zilieleza kuwa baadhi ya wawakilishi waliendelea kuonyesha misimamo mikali kuhusu baadhi ya masuala muhimu, wakisisitiza kuwa misimamo yao “inawakilisha matakwa ya pande wanazoziwakilisha.”

Masuala yaliyoibukia kuwa kiazi moto ni shinikizo za Azimio kuitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufungua sava za Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022, kujadiliwa kwa suala la gharama ya maisha na ukatili wa polisi dhidi ya waandamanaji.

Mrengo wa Kenya Kwanza, kwa upande wake, umeshikilia kuwa hautayajadili masuala hayo kwani “hayana umuhimu wowote kwa Wakenya”.

Kulingana na msimamo wa Kenya Kwanza, masuala ya uchaguzi mkuu yalikamilika wakati Azimio iliwasilisha kesi yake katika Mahakama ya Upeo, ambapo ilikubaliana na uamuzi wa IEBC, kwamba Rais William Ruto alichaguliwa kihalali.

  • Tags

You can share this post!

AMINI USIAMINI: Antpitta ni ndege mwenye soni akimwangalia...

Caroli Omondi: “Komeni kunitusi kwa jina la marehemu...

T L