• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 6:55 PM
Kimya kirefu cha Uhuru chazua maswali

Kimya kirefu cha Uhuru chazua maswali

NA WANDERI KAMAU

KIMYA kirefu cha Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, kimeibua maswali kuhusu aliko, wakati ambapo sauti na hata mchango wake unahitajika sana katika mrengo wa Azimio la Umoja.

Hadi sasa, Bw Kenyatta anahudumu kama mwenyekiti wa Baraza Kuu la mrengo huo, wadadisi wakisema hilo linamaanisha sauti yake ni muhimu, hasa unaposhiriki kwenye Mazungumzo ya Maridhiano yanayoendelea katika Ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Kando na nafasi hiyo, Bw Kenyatta alipewa jukumu la kuwa mpatanishi mkuu kwenye mizozo inayoendelea katika mataita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Ethiopia na Rais William Ruto, mara tu baada yake kumkabidhi uongozi Rais, Septemba 13 mwaka uliopita.

Baada ya uteuzi huo, alifaulu kuipatanisha serikali ya Ethiopia na waasi wa kundi la Tigray People’s Liberation Front (TPLF) nchini Ethiopia, kwenye mazungumzo yaliyofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini, Desemba 2022.

Katika mzozo wa DRC, Bw Kenyatta amekuwa akifanya vikao mbalimbali nchini humo, Kenya na nchini Uganda.

Mnamo Desemba, Bw Kenyatta alikutana na makundi 53 yanayozozana DRC katika hoteli moja jijini Nairobi, ambapo aliishukuru Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa juhudi ambazo imekuwa ikiendesha kusuluhisha mzozo huo.

Mnamo Mei, alihudhuria kikao kingine jijini Bunjumbura, Burundi, ambacho pia kilihusu mikakati ya kurejesha amani nchino DRC.

Mnamo Julai, aliongoza kongamano jingine jijini Goma, DRC, kuhusu hatua zilizopigwa kwenye mchakato huo.

Mwanzoni mwa mwezi uliopita, Agosti 8, 2023, Bw Kenyatta alikutana na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, jijini Kampala, kwenye kikao ambacho afisi yake ilikitaja kuwa juhudi za “kufuatilia mchakato wa amani nchini DRC”.

Tangu wakati huo, Bw Kenyatta amebaki kimya, ambapo hajaonekana hadharani tena.

Hapa Kenya, nyakati ambazo Bw Kenyatta alionekana hadharani ni Julai 24, 2023, alipofika katika makazi ya mtoto wake, Jomo Kenyatta, katika mtaa wa Karen, Nairobi, baada ya ‘kuvamiwa’ na polisi, wakidai kutafuta bunduki ‘haramu’ alizodaiwa kumiliki.

Kwenye kikao hicho—na kwenye mahojiano aliyofanya baadaye na vyombo vya habari—Bw Kenyatta aliilaumu serikali ya Rais Ruto kwa kuiingilia familia yake.

Nyakati nyingine alizoonekana hadharani ni Julai 28, alipoungana na kiongozi wa Azimio, Bw Raila Odinga, na viongozi wengine kuwakumbuka watu waliofariki kutokana na maandamano na Mei 22, alipoongoza mkutano wa Jubilee katika uwanja wa Ngong Racecourse. Pia, alionekana hadharani Aprili 26, baada ya afisi za chama hicho kuvamiwa na watu waliodaiwa kuunga mkono kambi ya mbunge Kanini Keeha wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Tangu Julai 28, Bw Kenyatta hajaonekana hadharani wala kusikika, maswali yakiibuka kuhusu aliko.

Kwenye mahojiano na wahariri wa vyombo tofauti vya habari, Bw Kenyatta alithibitisha kwamba yeye pamoja na familia yake wangesafiri nchini Uingereza kwa “likizo”, ijapokuwa “hilo halipaswi kufasiriwa kama kutoroka Kenya”.

“Nimekuwa na amani. Sijawahi kuwa na muda wa kutosha na familia yangu kama nitakavyo. Ukweli ni kuwa, ninataka kwenda kwenye likizo na watoto wangu pamoja na wajukuu wangu. Msiseme nimeitoroka nchi. Ninahitaji kupumzika, na wananihitaji,” akasema Bw Kenyatta.

Kutokana na ukimya huo mrefu, wadadisi wa siasa wanasema kuwa huenda ikawa kweli Bw Kenyatta alimaanicha alichosema, hasa baada ya kuhudumu karibu miaka kumi kama rais.

“Mwishoni mwa siku, wanasiasa pia ni watu. Pia, wao huhitaji kuwa pamoja na familia zao. Hata hivyo, nahisi kuwa Bw Kenyatta aliamua kuondoka nchini kwa muda kutokana na mazingira ya sasa ya kisiasa,” akasema Prof Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kwenye mahojiano, mdadisi huyo hata hivyo alisema kuwa hatua hiyo si nadra, kwani familia ya Kenyatta ina maslahi nchini Uingereza.

“Ni wazi kuwa familia ya Bw Kenyatta ina ukaribu mkubwa na Uingereza, kama historia inavyoonyesha tangu enzi ya utawala wa Mzee Jomo Kenyatta,” akasema Prof Munene.

Hata hivyo, mdadisi wa siasa Mark Bichachi anasema kuwa kuna uwezekano hatua ya Bw Kenyatta ilichangiwa na msukumo wa kisiasa. Anasema Bw Kenyatta alichukua hatua hiyo kutokana na usalama wa familia yake, hasa baada ya uvamizi wa shamba la Northlands (lililo Kaumti ya Kiambu) na hatua ya polisi ‘kuvamia’ makazi ya mwanawe.

“Matukio hayo mawili, bila shaka huenda ndiyo yalichangia Bw Kenyattta na familia yake kuondoka, japo Bw Kenyatta hakusema hilo kwa njia ya wazi,” akasema.

Wadadisi pia wanasema hatua ya Bw Kenyatta inalenga kuondoa taswira ambayo imekuwa ikibuniwa na mrengo wa Kenya Kwanza,  kwamba ndiye amekuwa akifadhili maandamano ambayo yamekuwa yakiendeshwa na Azimio.

Hata hivyo, wanaonya kuwa kwa Bw Odinga, ukimya huo unamwacha mpweke kisiasa, kwani anaonekana “kutekeleza majukumu ya Upinzani peke yake”.

“Kitaswira, ukimya wa Bw Kenyatta si mzuri, kwani wafuasi wa Bw Odinga wanahisi hamuungi mkono kikamilifu,” asema mdadisi Oscar Plato.

  • Tags

You can share this post!

Karen Nyamu: Ruto ndiye ameumia zaidi na kupanda kwa bei ya...

Seneta achemkia wanawake kwa kukataa Sh500 za motisha ya...

T L