• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Kioni: Uhuru hajaitisha mtu pensheni

Kioni: Uhuru hajaitisha mtu pensheni

NA BENSON MATHEKA

RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta huenda akaamua kuacha pensheni yake kama rais wa nne wa Jamhuri ya Kenya na hafai kushinikizwa kuacha kushiriki siasa, katibu wa chama cha Jubilee anayepigwa vita Jeremiah Kioni amesema.

Bw Kioni amekosoa hatua ya mrengo unaompiga vita pamoja na Bw Kenyatta akisema katiba inamtaka rais mstaafu kuacha wadhifa wa chama cha kisiasa ili aweze kupata pensheni na marupurupu yake pekee na wala sio katiba ya chama hicho.

“Iwapo hajadai pensheni yake, kwanini anasumbuliwa,” alisema Bw Kioni akihutubia wanahabari katika makao makuu ya chama cha Jubilee kinachokumbwa na mzozo wa uongozi.

Mrengo wa chama hicho unaoongozwa na mbunge maalumu Sabina Chege na mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega umemtimua Bw Kenyatta kama kiongozi wa Jubilee ukisema aliacha wadhifa huo miezi sita baada ya kuondoka mamlakani.

Bi Chege amedai kutwikwa wadhifa wa kaimu mwenyekiti wa chama hicho huku Bw Kega akidai kumpokonya Bw Kioni wadhifa wa katibu mkuu.

Wiki jana, mrengo wao kupitia ilani kwenye magazeti na mitandao ya kijamii iliyotiwa saini na Bw Kega, ilifutilia mbali mkutano wa Baraza la Kitaifa la Wajumbe (NDC) ambao Bw Kenyatta aliitisha wakidai hakuwa na mamlaka ya kufanya hivyo kwa kuwa kulingana nao, alikoma kuwa kiongozi wa chama mwezi Machi. Jana, Bw Kioni alisisitiza kuwa mkutano huo utafanyika ulivyopangwa Mei 22 na 23.

“Tumepata ufafanuzi kuhusu suala ya kiongozi wa chama (Uhuru Kenyatta), wale wanaosema kwamba ni lazima ajiuzulu, baadhi hata wamedanganya. Suala la kujiuzulu kushiriki siasa liko katika sheria ya pensheni, na kama hajakuitisha pensheni, shida yako ni gani? Si ukae na pensheni na yeye aendelee na maisha yake,” Bw Kioni alisema.

Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragwa alisisitiza kuwa Bw Kenyatta ndiye kiongozi wa Jubilee na mwenyekiti wa Baraza Kuu la muungano wa upinzani wa Azimio “Tuko katika Azimio ilivyokubaliwa katika NDC na ni kupitia NDC ambapo uamuzi wa kujiondoa unaweza kufanywa,” alisema.

Mrengo unaompiga vita Bw Kenyatta unaegemea muungano unaotawala wa Kenya Kwanza ambao umekuwa ukimlaumu rais mstaafu huyo kwa kufadhili maandamano ya Azimio. Alipuuza ilani ya kufutilia mbali mkutano wa NDC akisema utafanyika jijini Nairobi.

“Kuna mambo mengi yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na pia katika magazeti ikiwemo ilani ya hivi majuzi ambapo baadhi ya watu walidai kufutilia mbali NDC. Ni muhimu kuwafahamisha wanachama wetu kwamba NDC itafanyika Mei 22 na 23 alivyotangaza kiongozi wa chama chetu. Kwa hivyo, wapuuze habari zingine zozote watakazoona popote ikiwemo katika magazeti,” alisema Bw Kioni.

  • Tags

You can share this post!

Dhambi za Yesu wa Tongaren kulingana na polisi

Unga nafuu kuzidi kuadimika sokoni

T L