• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Kivumbi leo Azimio wakiapa kuingiza wafuasi katikati mwa jiji

Kivumbi leo Azimio wakiapa kuingiza wafuasi katikati mwa jiji

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Azimio Raila Odinga jana Jumatatu alisisitiza kuwa wafuasi wao hawatabeba silaha au kuhusika na vitendo vyovyote vya ghasia na uharibifu wa mali katika maandamano ya leo ambayo serikali imeharamisha.

Bw Odinga alisema maandamano yao katikati ya jiji ya Nairobi yataanza saa kumi na mbili asubuhi na lengo lao ni kuwasilisha malalamishi katika ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Afisi ya Rais, Wizara ya Fedha na Tume ya Utumishi wa Umma.

“Tunathibitisha kwamba maandamano yatakuwa kesho kuanzia saa kumi na mbili asubuhi. Kama tulivyosema, Katiba inapatia kila mtu haki ya kuandamana kwa amani na bila silaha, kukusanyika na kuwasilisha malalamishi kwa afisi za umma,” Bw Odinga alisema katika taarifa akiandamana na vinara wenza wa Azimio miongoni mwao Kalonzo Musyoka, Martha Karua na Jeremiah Kioni.

Raila alilaumu polisi kwa kupiga marufuku maandamano hayo akisema kamanda wa polisi wa Nairobi hana mamlaka ya kufanya hivyo kwa kusingizia kwamba wafuasi wa Azimio walibeba silaha na kuharibu mali upinzani ulipoandamana wiki tatu zilizopita.

“Waandamanaji wetu kesho wamefahamishwa kwamba maandamano yatakuwa ya amani. Hakuna anayeruhusiwa kubeba silaha yoyote. Hakuna anayefaa kuvamia biashara ya kibinafsi ya mtu. Tunachofanya ni kuandamana kuwasilisha malalamishi yetu kwa maafisa husika wa serikali,” alisema.

Hata hivyo, jana Jumatatu, Naibu Inspekta Jenerali wa polisi Noor Gabow alisisitiza kuwa maandamano hayo ni marufuku na hayataruhusiwa kwa vyovyote vile.

Kwenye taarifa kwa wanahabari, Bw Gabow alisema ingawa katiba inapatia Wakenya haki ya kuandamana kwa amani na bila silaha na hata kuwasilisha malalamishi kwa maafisa wa serikali, maandamano ya Azimio yamekuwa yakikumbwa na ghasia na uharibifu wa mali na sheria inapatia polisi jukumu la kuilinda.

“Kwa sababu za usalama wa taifa, tunataka kufahamisha umma kwamba maandamano yaliyopangwa au mkutano huo ni kinyume cha sheria na kusisitiza kauli yetu ya awali ya kulaani maandamano ya ghasia na mashambulizi dhidi ya maafisa wa usalama,” alisema Bw Gabow.

Msimamo wa polisi unafuatia onyo la Rais William Ruto kwamba atatumia nguvu zake kama amiri mkuu wa majeshi kuzima maandamano ya Azimio akisisitiza kuwa lengo la upinzani ni kuharibu biashara jijini Nairobi.

Bw Odinga anasema polisi hawawezi kuamua kutakuwa na ghasia kabla ya maandamano kufanyika na kisha kupiga marufuku shughuli za kisiasa zinazoruhusiwa na katiba.

“Hizi ni ishara za udikteta. Ni sawa na kuweka kando katiba na hatutakubali,” aliongeza.

Kiongozi huyo wa ODM alisema serikali ikiruhusiwa kutumia vitisho kuzima haki za kikatiba za Wakenya hali itakuwa mbaya.

Alisema mazungumzo ya maridhiano yalisambaratika kwa kuwa Kenya Kwanza haikuwa na nia njema kwa kile alichosema kuendelea kuua demokrasia ya vyama vingi.

  • Tags

You can share this post!

Waziri Kuria: Tutapeleka maandamano kwa Kenyatta

Ahadi ya Ruto kuhusu bei ya unga sasa yatamausha

T L