• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 PM
Kupe wa kisiasa wamfyonza Ruto

Kupe wa kisiasa wamfyonza Ruto

BENSON MATHEKA NA CHARLES WASONGA

?WASHIRIKA wa Naibu Rais William Ruto wamegeuka kupe kwa ‘ kufyoza mamilioni ya fedha anazoyapa makundi ya ‘walalahoi’ kote nchini katika kampeni za kusaka kura za urais katika mwaka wa 2022.

Ni tabia yao hiyo inayosababisha wanachama wa makundi ya ‘mahasla’ mfano wa bodaboda na mama-mboga kuzua fujo katika kaunti ambazo Dkt Ruto amekuwa akizuru.Kaunti ambazo mahasla wameshiriki ghasia wakilalamikia kulaghaiwa fedha wanazopewa na Naibu Rais katika mpango wake wa kuwawezesha ni Meru, Bomet, Bungoma, Kajiado, Tharaka Nithi, Machakos, Tharaka Nithi, Kisumu na nyingine.

Polisi wameshutumu ongezeko la visa vya wanachama wa makundi hayo kuzua fujo wakidai kupunjwa fedha na washirika wa Dkt Ruto, wakisema ni tishio kwa amani katika maeneo husika.Mwezi jana, Msemaji wa Polisi, Bruno Shioso alihusisha ghasia zilizokumba ziara ya Dkt Ruto katika eneo la Kondele, Kisumu, na malalamishi kuhusu Sh2 milioni alizotoa zigawiwe bodaboda na makundi ya wafanyabiashara wadogo.

Dkt Ruto huandamana na washirika wake kutoka maeneo anayotembelea wanaomsaidia kuandaa mikutano na mama-mboga, bodaboda na wachuuzi.Kulingana na wadadisi, washirika wa Dkt Ruto wamegeuza kampeni yake kuwa njia ya kumfyonza pesa wakidai wanazitumia kustawisha watu wa mapato ya chini.

“Wanang’ang’ana kuandaa mikutano ili watumie ukarimu wa Dkt Ruto kupata pesa wakidai wanasaidia maskini ilhali wanajaza mifuko yao. Hii ndiyo sababu unaona ghasia kila eneo analotoa pesa,” asema David Kinyanyui, mdadasi wa siasa.

Ikizingatiwa Dkt Ruto amekuwa akiendeleza kampeni yake ya kuwawezesha kiuchumi walalahoi kwa takriban miaka minne sasa, washirika wake wanaopokea pesa hizo huzitia mfukoni kwa maelfu ya mamilioni.Mnamo Novemba 17, ghasia zililipuka katika eneo-bunge la Tigania Mashariki, Kaunti ya Meru baada ya Sh1 milioni walizopewa na Naibu Rais kutoweka.

Bodaboda waliwasha moto katika soko la Muriri lililoko barabara ya Meru-Maua huku baadhi yao wakidai mbunge wa eneo hilo Gichunge Kabeabea alitia mfukoni sehemu za fedha hizo.Hata hivyo, meneja wa afisi ya Hazina ya Ustawi wa Eneobunge la Tigania Mashariki, Lawrence Mutwiri alikana madai hayo akiyahusisha na njama ya kuharibia Bw Kubeabea sifa kwa ajili ya uchaguzi ujao.

“Wanaoeneza propaganda hizo za kumharibia jina mbunge wetu ni wapinzani wake. Wao ndio wameandaa maandamano hayo ambayo pia yanaharibu jina la Naibu Rais,” Mutwiri akaripotiwa akisema.Alitoa wito kwa Dkt Ruto kupitisha pesa kama hizo mikononi mwa “viongozi wangwana na waadilifu”.

Katika Kaunti ya Bungoma, makundi ya mama-mboga na boda boda yalilalamika kulaghaiwa Sh2 milioni walizozawadiwa na Naibu Rais alipowahutubia katika soko la Chepkube.?Kabla ya hapo Dkt Ruto alikuwa amezuru maeneo bunge ya Tongaren, Webuye Mashariki, Kimilili, Kabuchai, Mlima Kenya, Sirisia, Bumula na Webuye ambapo alitoa jumla ya Sh15 milioni za kupiga jeki biashara zao.

Mnamo Oktoba, wanachama wa makundi mbalimbali ya bodaboda walizua rabsha katika kaunti za Kajiado na Murang’a wakidai kupunjwa na wabunge wao waliopokea pesa walizozawidiwa na Naibu Rais.Jana, wabunge kadhaa wanaoegemea chama chaUDA tuliosaka kauli zao kuhusu suala hilo walikataa kuligusia isipokuwa mmoja wao aliyeomba tusitaje jina lake.

“Pesa ambazo Naibu Rais amewahi kutoa katika eneobunge langu nimehakikisha zimewafikia walengwa. Ikiwa kuna wale ambao ‘hulalia’ pesa hizo basi ni shauri yao,” mbunge mmoja kutoka magharibi mwa Kenya, ambaye aliomba tulibane jina alijibu kupitia ujumbe.

You can share this post!

Mutua aahidi wanandoa ‘zawadi’ ya Sh0.5 milioni...

AC Milan watua kileleni mwa Serie A baada ya Atalanta...

T L