• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 4:47 PM
Kuzikwa kwa BBI kwageuka pigo kwa Moi Bondeni

Kuzikwa kwa BBI kwageuka pigo kwa Moi Bondeni

Na FRANCIS MUREITHI

KUSAMBARATIKA kwa Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI) kumefifisha pakubwa ushawishi wa kisiasa wa mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi, katika eneo la Bonde la Ufa.

Hili ndilo pigo la pili la kisiasa la dhidi ya Bw Moi katika azimio lake la kumrithi Rais Uhuru Kenyatta, baada ya Bunge la Kaunti ya Baringo kuwa la kwanza kuuangusha mswada huo.

Kuharamishwa kwa BBI na Mahakama ya Rufaa kunaonekana kama ushindi mkubwa kwa Naibu Rais William Ruto, kwenye juhudi za kuimarisha ushawishi wake wa kisiasa katika eneo la Bonde la Ufa.Kulingana na mdadisi wa siasa Joseph Ngugi, kuharamishwa kwa mpango huo ni kama mapinduzi ya kisiasa dhidi ya Gideon.

“Kufuatia kuharamishwa kwa BBI, Dkt Ruto sasa anaonekana kama ndiye hasa kiongozi wa kisiasa wa jamii ya Wakalenjin. Kufutiliwa mbali kwa BBI ni pigo kwa Gideon, ikizingatiwa alitarajiwa kutwaa uongozi wa jamii hiyo kutoka kwa baba yake, marehemu Daniel Moi,” akasema Bw Ngugi.

Aliongeza, “Katika hali hiyo, mwelekeo wa kisiasa wa Gideon unayumba katika kaunti hiyo na katika ngazi ya kitaifa. Haonekani kuwa na ushawishi wowote ikiwa kutaibuka hali ambapo atajiunga na miungano ya kisiasa. Ushawishi wake kwa sasa huenda ukawa tu uwezo mkubwa wa kifedha alio nao.

”Hata hivyo, mbunge William Kamket (Tiaty), ambaye ni kati ya washirika wa karibu wa Gideon, Seneta huyo hakupoteza chochote kutokana na ‘kifo’ cha BBI.

“Hakupoteza lolote. Badala yake, hali hiyo ni kama baraka kwake, kwani atapata muda wa kutosha kupiga jeki juhudi zake kupigania tiketi ya urais ya muungano wa OKA 2022,” akasema Bw Kamket na kuongeza: “Kama mwanachama wa OKA, Gideon ana uungwaji mkono mkubwa kote nchini.”

“Hili ni kinyume na Dkt Ruto, ambaye anategemea eneo la Bonde la Ufa pekee. Gideon anahitaji tu kuidhinishwa kama mgombeaji-urais wa OKA. Baada ya hilo, wenyeji wa Bonde watakuwa na nafasi ya kuamua ni nani anayefaa zaidi kuwa rais kati ya Gideon na Dkt Ruto 2022. Hilo ndilo tunangoja.”

Badala yake, mbunge alieleza kuwa kuanguka kwa BBI ni pigo kwa Dkt Ruto kwenye juhudi za kiumarisha uungwaji mkono wake Bondeni.

You can share this post!

Ole Lenku aenda Uarabuni kuokoa msichana anayeteswa

Ruto asema kamwe hatajiuzulu