• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Mabwanyenye wa Mt Kenya leo ‘kupitisha’ Raila

Mabwanyenye wa Mt Kenya leo ‘kupitisha’ Raila

Na KENNEDY KIMANTHI

MABWANYENYE wa eneo la Mlima Kenya leo wanatarajiwa kumwidhinisha rasmi kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kama mgombea urais watakayemuunga mkono kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Mabwanyenye hao watatoa tangazo hilo chini ya mwavuli wa Wakfu wa Mlima Kenya (MKF), siku moja kabla ya Bw Odinga kuzindua azma yake Ijumaa. Wakfu huo umekuwa ukihusika pakubwa kwenye siasa za urithi katika eneo hilo kwenye chaguzi zilizopita.Duru ziliiambia ‘Taifa Leo’ mabwanyenye hao vile vile watamtangaza mgombea-mwenza wa Bw Odinga, Februari mwaka ujao.

Mkutano wa kumwidhisha Bw Odinga utafanyika leo, jijini Nairobi, ambapo utahudhuriwa na wanasiasa kutoka Mlima Kenya, wanawake, vijana, viongozi wa kibiashara na kidini. Watakutaka katika hoteli ya Safaripark, sawa na vikao walivyofanya awali.

Jana, Naibu Mwenyekiti wa wakfu huo, Bw Titus Ibui, aliiambia ‘Taifa Leo’ kwamba kundi hilo limemaliza mchakato wa kumtafuta yule atakayemrithi Rais Uhuru Kenyatta. Kwa sasa, eneo la Mlima Kenya halina mwanasiasa mwenye ushawishi kumrithi Rais Kenyatta, muhula wake unapokaribia kukamilika Agosti, mwaka ujao.

Alisema kundi hilo limetathmini sera za Bw Odinga kuhusu Mlima Kenya na kuamua ndiye anayefaa zaidi miongoni mwa wawaniaji waliojitokeza kugombea urais. Alisema kuwa kwa sasa wanapanga jinsi atakavyoingia uongozini uchaguzi huo unapoendelea kukaribia.

Bw Odinga anatarajiwa kuzindua rasmi azma yake kuwania urais kwenye mkutano wa Mpango wa Azimio la Umoja uliopangiwa kufanyika katika Uwanja wa Kasarani, Ijumaa. Bw Ibui alithibitisha wanachama wa MKF watahudhuria. “Lazima Mlima utoe sauti yake.

Tulipo sasa, tumefanya uamuzi wetu na tutakabidhi masuala ya kisiasa kwa viongozi wetu. Tumewaambia baadhi yao kuhusu msimamo wetu. Mtasikia kutoka kwetu Jumatano (leo) wakati tangazo hilo litakapotolewa,” akasema Bw Ibui.

Kutokana na ushawishi wao mkubwa wa kisiasa na kiuchumi, tangazo la mabwanyenye hao linatarajiwa kugeuza mkondo wa kisiasa katika ukanda huo.Katika siku za hivi karibuni, wakfu huo umekuwa ukiendesha juhudi za kumpigia debe Bw Odinga katika eneo hilo.

Lilisema linaamini Bw Odinga ndiye atashughulikia maslahi yake kikamilifu, hasa kutokana na ukaribu ambao amekuwa na Rais Kenyatta tangu walipobuni handisheki mnamo 2018.Kundi pia limekuwa likijaribu kuondoa dhana kwamba Bw Odinga si maarufu katika eneo hilo.

Juhudi zake zimepata uungwaji mkono wa idadi kubwa ya magavana.Magavana wanaomuunga mkono Bw Odinga ni Kiraitu Murungi (Meru), Lee Kinyanjui (Nakuru), Martin Wambora (Embu), Ndiritu Muriithi (Lakipia), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi), James Nyoro (Kiambu) na Francis Kimemia (Nyandarua).

Katika siku za hivi karibuni, Rais Kenyatta pia amekuwa akionyesha ishara za kumuunga mkono Bw Odinga kwenye semi zake.

You can share this post!

JUMA NAMLOLA: Tulitelekeza watoto wetu kwa muda mrefu, sasa...

Utata kuhusu idadi ya waliofariki Mto Enziu

T L