Siasa

Macho kwa Ruto akipamba sherehe za ODM

Na JUSTUS OCHIENG November 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MACHO yote sasa yameelekezwa kwa Rais William Ruto huku akipanga kuhudhuria sherehe ya kuadhimisha miaka 20 ya chama cha ODM, tangu kuundwa kwa chama hicho.

Hatua hiyo sasa inaonekana kama njama ya kupata wapiga kura wa ngome za aliyekuwa waziri mkuu hayati Raila Odinga uchaguzi wa 2027 ukikaribia.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema macho yote yatalenga Kiongozi huyo wa  Nchi, ambaye alikuwa na ukuruba  na Raila  hasimu wake wa kisiasa  huku akijiunga na waanzilishi wengine wa ODM katika sherehe za miaka 20 za chama hicho za siku nne mjini Mombasa.

“Hii ishara ya kisiasa inatarajiwa kuanzisha mpangilio mpya kabla ya uchaguzi wa 2027,” anasema mchambuzi wa kisiasa Dismas Mokua.

Mbali na Rais Ruto, waanzilishi wengine wa  chama chicho walioalikwa  kuhudhuria sherehe hizo kuanzia Alhamisi Novemba 13, wakati wa kikao maalum cha Baraza Kuu la Taifa (NGC), hadi Jumapili Novemba 16, ni pamoja na Rais  mstaafu Uhuru Kenyatta,  Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, wanachama waanzilishi Najib Balala na Charity Ngilu, mwenyekiti wa kwanza Henry Kosgei na Katibu Mkuu wa kwanza, Prof Anyang’ Nyong’o ambaye ni Gavana wa Kisumu.

Wengine ni Spika wa zamani wa Bunge la Kitaifa Kenneth Marende, mawaziri wa zamani Franklin Bett na Fred Gumo, mawaziri Hassan Joho (Madini) na Wycliffe Oparanya (Ushirika), mwanzilishi wa ODM Mugambi Imanyara ambaye alimkabidhi Odinga chama baada ya kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, kuondoka na ODM-Kenya, pamoja na wageni wengine.

Bw Musyoka pia alialikwa kwenye sherehe hizo na Raila kabla ya waziri mkuu huyo wa zamani kufariki, lakini alikataa.

“Niliona Raila amenitumia barua akinialika kwenye ODM@20. Sitahudhuria. Nawatakia kila la kheri. Nimetumia sehemu kubwa ya maisha yangu kuunga mkono Raila,” alisema mnamo Septemba.

Maadhimisho haya, kulingana na kaimu  kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga, yatachanganya sherehe na tafakari, ikiwa ni mchanganyiko wa ishara ya kuomboleza na kuanza upya huku chama kikiweka mwelekeo baada ya Raila kabla ya uchaguzi wa 2027.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi, Junet Mohamed alisema: “Timu ya ODM itaondoka Nairobi Alhamisi Novemba 13 saa 2 asubuhi kwa kutumia SGR kuelekea Mombasa.”

Chama kisha kitaanza sherehe zake za siku nne kuadhimisha miaka 20 tangu kuundwa kwake, kipindi kilichojikita katika mapambano ya kisiasa, kujitolea, na huduma kwa Wakenya – na sasa kimekumbwa na kifo cha kiongozi wake wa kwanza, Raila Odinga.

Dkt Oginga, alisema maadhimisho hayo yatajumuisha mikutano ya kisiasa, mazungumzo kati ya vizazi, tamasha za muziki, na ibada ya shukrani kuenzi kumbukumbu ya Odinga na harakati alizojenga.

“ODM@20 si alama tu ya muda – ni kufufua ahadi yetu ya kutetea demokrasia, kulinda uhuru tuliopata kwa gharama kubwa, na kuendelea kupigania usawa, haki za kijamii na Kenya kwa wote,” alisema Dkt Oginga katika taarifa iliyotolewa Jumatatu.

Maadhimisho yanaanza na kikao maalum cha Baraza Kuu la Taifa (NGC) Alhamisi Novemba 13, ambapo mashirika ya chama yatachambua miaka 20 ya uanaharakati wa kisiasa na kujadili mwelekeo wa harakati hizo katika enzi ya baada ya Raila.

NGC pia itathibitisha viongozi wa muda ikiwa ni pamoja na Dkt Oginga, mwenyekiti Gladys Wanga na makamu wake wenzake; Abdulswamad Nassir, Godfrey Osotsi na Simba Arati