• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
Matusi ya viongozi yaaibisha serikali

Matusi ya viongozi yaaibisha serikali

NA BENSON MATHEKA

HUKU serikali ya Jubilee ikikaribia kuondoka mamlakani baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, viongozi wake wameonyesha ukosefu mkubwa wa adabu kwa kutusiana hadharani.

Kwa kawaida, maafisa na viongozi wakuu wa serikali wanapaswa kudumisha viwango vya juu vya heshima na nidhamu kwa wakubwa wao na kuepuka matamshi yanayoweza kuanika udhaifu wowote wa kimamlaka.

Hata hivyo, viongozi wa serikali wanazidi kuanika wazi jinsi ukosefu wa heshima ulivyojikita katika serikali ya Jubilee kwa miaka tisa ambayo imekuwa mamlakani wakilaumiana, kudharauliana na kuumbuana hadharani.

Kuanzia Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto hadi mawaziri, viongozi na maafisa wa serikali wanaonekana kutumia kipindi hiki cha lala salama cha kampeni za uchaguzi mkuu kuvuana nguo wakilumbana kwa matamshi ambayo baadhi hayawezi kuchapishwa.

Hali hii ilishika kasi baada ya kanda kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii iliyomnukuu Dkt Ruto akisimulia alivyokasirishwa na mkubwa wake Rais Kenyatta hadi akawazia kumchapa kofi kwa kutaka kuacha uongozi Mahakama ya Juu ilipofuta ushindi wake mnamo 2017.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, matamshi ya Dkt Ruto, ambayo hakukanusha, na matukio kadhaa yaliyofuatia na yaliyotangulia, yanaonyesha kiwango ambacho serikali ya Jubilee imekosa adabu na nidhamu ya ndani.

“Kwa kutumia lugha inayoonyesha ukosefu wa heshima kiasi cha kuwazia kuchapa kofi mkubwa wako ambaye ni kiongozi wa nchi na kuwa na ujasiri wa kueleza hivyo mbele ya kundi la watu, ni kuonyesha msingi ambao serikali ya Jubilee ilijengwa,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Anasema ilikuwa makosa kwa Rais Kenyatta kuingilia suala hilo.

Rais Kenyatta amekuwa akimfokea Dkt Ruto hadharani japo ana uwezo wa kumuagiza akomeshe lugha isiyo na heshima.

Dkt Gichuki anasema msingi huu ulibainika mwanzo wa muhula wa pili Rais Kenyatta alipomtaja Dkt Ruto kama mtu wa kutangatanga.

UTOVU WA ADABU

“Mirengo miwili iliyozuka mwanzoni mwa muhula wa pili wa utawala wa Jubilee ya Tangatanga na Kieleweke iliweka msingi ambao umechangia hali inayodhihirika kwa wakati huu,” asema.

Dkt Ruto na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa ni viongozi wa hivi punde kuonyesha ukosefu wa adabu, baada ya waziri huyo kudai kwamba nusura naibu rais amchape kofi kwa kupeleka ujumbe wa viongozi wa eneo la Magharibi katika Ikulu.

Matamshi ya Bw Wamalwa akiwa kwenye mkutano wa kampeni wa Azimio la Umoja katika uwanja wa Bukhungu, Kakamega yamezua msururu wa mashambulizi baada ya Dkt Ruto kumjibu kwa lugha isiyo ya heshima.

Jumatano, Bw Wamalwa alimtaka Dkt Ruto kukoma kumtusi katika kampeni zake kaunti za Bungoma na Trans Nzoia.

“Sijawahi kumtusi na sielewi ni kwa nini ananichokoza nianze kufanya hivyo,” alisema na kufichua kwamba Dkt Ruto alipinga kuteuliwa kwake kuwa waziri.

Japo mawaziri na makatibu wa wizara wanapaswa kumheshimu Dkt Ruto akiwa msaidizi rasmi wa rais, baadhi wamekuwa wakimpuuza na kutumia lugha isiyofaa wakimtaja kama mfisadi na asiye na heshima bila kuthibitisha madai hayo.

Mnamo Septemba 2020, Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko, alishambuliana hadharani na Dkt Ruto kwa kumwita karani wa rais.

“Naibu Rais anafaa kuwa karani wa rais. Jinsi ninavyoheshimu rais kama karani wake, ndivyo naibu rais na washirika wake wanapaswa kumheshimu rais,” Bw Tobiko alisema katika mkutano alioandamana na wenzake Dkt Fred Matiang’i na Mutahi Kagwe.

Dkt Ruto na washirika wake pia wamekuwa wakitumia lugha isiyo ya heshima kwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, Katibu wa wizara hiyo Karanja Kibicho na wakuu wa idara za usalama kama Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai na Mkurugenzi wa DCI George Kinoti.

Wiki mbili zilipita, Dkt Ruto alisema Bw Mutyambai ndiye mkuu wa polisi ovyo zaidi ulimwenguni akisema anafuata maagizo kutoka kwa rais.

Jana Jumatano, Dkt Matiang’i alimuonya Ruto dhidi ya kuendelea kushambulia maafisa wakuu wa usalama nchini.

Visa vya ukosefu wa adabu pia vimeshuhudiwa baina ya idara za serikali kama vile Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwa wakuu wa idara hizo kushambuliana hadharani badala ya kusuluhisha tofauti zao kwa njia rasmi.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Rais akumbuke IDPs waliotengewa vipande...

TAHARIRI: Wakenya watatoa uamuzi wa mwisho kuhusu wanasiasa...

T L