• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Mnikumbuke wiki ijayo, Raila asihi

Mnikumbuke wiki ijayo, Raila asihi

NA JAMES MURIMI

MWANIAJI urais wa chama cha Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga anasisitiza kuwa Wakenya wanapaswa kuchagua kati ya viongozi watakaoleta mabadiliko na wale ambao wanahusishwa na kashfa za ufisadi, wakati wa uchaguzi wiki ijayo.

Akiandamana na mgombea wake mwenza, Bi Martha Karua na viongozi wengine kwenye kampeni zao maeneo ya Kerugoya, waliwaonya Wakenya dhidi ya kumpigia kura mgombeaji urais wa Kenya kwanza William Ruto.

Bw Odinga alisema muungano wake ndio unafaa zaidi kuendesha nchi na kuleta maendeleo baada ya kuondoka kwa Rais Uhuru Kenyatta mamlakani.

“Wakenya wako katika njia panda katika uchaguzi ujao. Ni wakati wao wa kuchagua kati ya mwelekeo wa ufisadi na wa maendeleo. Uchague kwa busara au uendelee kubaki nyuma kama nchi. Tunawaomba wote muamke mapema na kupiga kura kwa mimi na Karua,” akasema kiongozi huyo wa chama cha ODM.

“Ikiwa mtatupigia kura kwa wingi Agosti 9, mimi na Karua tutaapishwa na tutakuwa na Kenya mpya,” akaongeza.

Alimshutumu mgombea mwenza wa Dkt Ruto ambaye ni Rigathi Gachagua kwa ufisadi na kukusanya mabilioni ya pesa za umma.

“Mgombea mwenza wa Bw Ruto Rigathi Gachagua hivi majuzi alishtakiwa kwa kuiba Sh200 milioni ambazo ni mali ya serikali. Mtu wa hali hii ni mfano wa kuwa mwizi. Alikuwa mbunge mara moja lakini katika kipindi cha uongozi wake, Sh13 bilioni zimewekwa kwenye akaunti yake. Ikitokea mmekutana naye, muulize chanzo cha utajiri huo,” Bw Odinga alisema.

“Nilisikia Gachagua aliwahi kuwa Ofisa wa Wilaya, alipataje hizo Sh13 bilioni? Ndio maana nasisitiza tudhibiti wizi wa rasilimali za umma na kuchochea maendeleo katika nchi hii. Hili linaweza kufikiwa,” aliongeza.

Kwa upande wake, Bi Karua alitumia jukwaa hilo kuleta maelewano mwafaka kati ya Bw Charles Kibiru wa (Jubilee) na Muriithi Kagai wa (Narc Kenya) ambao wanawania kiti cha ugavana katika kaunti ya Kirinyaga chini ya muungano wa Azimio la Umoja.

Kiongozi huyo wa chama cha Narc Kenya alisema anawasiliana na Bw Odinga ili kuhakikisha kuwa maafikiano ili kupata mgombea mmoja wa kiti hicho uchaguzini. katika uchaguzi ujao.

“Azimio imeleta pamoja zaidi ya vyama 26 vya kisiasa vinavyolenga kuwaleta pamoja watu wote kutoka pembe zote za jamhuri hii. Lakini tumetengana hapa Kirinyaga kuhusiana na kinyang’anyiro cha ugavana. Tuna watoto wawili wa Azimio hapa Kirinyaga ambao ni wa Jubilee na Narc Kenya. Mimi ni mama yao. Mimi na Odinga ni wazazi wao,” akasema Bi Karua.

Alionya kuwa muungano huo utapoteza kiti hicho kwa Kenya Kwanza ikiwa utawasilisha wagombea wawili.

“Wajumbe wa pande hizo mbili watakutana ili kuamua nani awe mpeperushaji bendera kati ya Kagai na Charles Kibiru. Ikiwa kutakuwa na wagombea wawili wa Azimio, tutapoteza uchaguzi huu na kupata aibu. Kiti cha ugavana ni muhimu zaidi na lazima nihakikishe kuwa kuna maafikiano,” Bi Karua alisema.

“Mungu yuko upande wetu na nina matumaini kuwa tutachaguliwa kuongoza nchi hii Jumanne ijayo. Ikiwa hatutapata gavana wa Azimio kwenye uwanja wangu wa nyuma, nitakuwa nikiwasiliana na nani ili kujadili mambo yanayohusu maendeleo?’ aliongeza.

Waziri wa Kilimo Peter Munya aliunga mkono uungwaji mkono wa Bw Odinga, akisema kwamba ana uwezo wa kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kubadilisha uchumi wa nchi.

“Chini ya uongozi wa Raila, tutaendelea kutekeleza mageuzi katika sekta ya kilimo. Ni lazima tupigane na tatizo hili linaloitwa ufisadi,” akasema Bw Munya.

Munya alisema, ofisi yake inachunguza wauzaji ambao wanauza unga wa mahindi zaidi ya Sh100, akisisitiza kuwa wizara yake ya kilimo imewalipa ipasavyo.

“Tumewalipa wahusika wa mahindi wote lakini baadhi yao wanajaribu kuficha unga wa mahindi na ushuru kutoka kwa wakenya. Ofisi yangu inachunguza suala hilo na tutawachukulia hatua wahusika hao na kuhakikisha kuwa unga unauzwa kwa Sh100,” akasema.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth alimwambia Naibu wa Rais kukubali kushindwa, akisema kuwa Raila na Karua watashughulikia maslahi yake ikiwa watashinda uchaguzi.

“Nchi nzima inajiandaa kwa urais wa Raila Odinga. Viashiria vyote vinaonyesha kuwa Raila atashinda uchaguzi huu na washindani wetu wana nia ya kupata kura za huruma kwa kudai kuwa maisha yao yako hatarini.” Bw Kenneth alisema.

“Tunapochukua uongozi wa nchi hii, tutalinda maslahi yao. Wanafaa kukoma kueneza propaganda kwa Wakenya kwa sababu wataenda nyumbani na Rais Kenyatta,” akaongezea.

Mwakilishi wa Kike wa Murang’a Sabina Chege, aliwataka wakazi hao kuunga mkono mgombeaji Bi Karua na kuhakikisha kwamba anakuwa naibu wa rais wa kwanza mwanamke baada ya Agosti 9.

“Wiki ijayo, nchi itakuwa ikiwatazama kwa makini watu wa Kirinyaga na tunatumai kuwa mtamchagua naibu rais wa kwanza mwanamke,” akasema Bi Chege.

You can share this post!

Shangwe na hoihoi Lee Njiru akizindua kitabu kuhusu ikulu

Ipsos: Raila kifua mbele huku zikisalia siku 6

T L