• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
Mrengo wa tatu wa kisiasa waibuka Bondeni

Mrengo wa tatu wa kisiasa waibuka Bondeni

Na BARNABAS BII

MRENGO wa tatu wa kisiasa umeibuka katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, hali ambayo imezua mgawanyiko mkubwa baina ya wazee wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto na Seneta Gideon Moi (Baringo).

Wawili hao wamekuwa wakimenyania hadhi ya anayepaswa kuwa kiongozi kwa kisiasa wa jamii hiyo, uchaguzi mkuu wa urais wa 2022 ukiendelea kukaribia.

Mrengo wa tatu unaojiita ‘Team Diaspora’ unashirikisha wanasiasa na viongozi kutoka jamii tofauti katika eneo hilo.

Wanachama wengi wa mrengo huo hawatoki katika jamii ya Wakalenjin.

Wadadisi wanatabiri kuwa, huenda mrengo huo ukaleta mwelekeo mpya wa kisiasa katika ukanda huo, huku watu wengi wakiendelea kutangaza nia ya kuwania nyadhifa mbalimbali za kisiasa.

Mrengo huo pia unatabiriwa kuathiri matokeo ya uchaguzi katika ukanda huo, kulingana na mwelekeo ambao utafuata.

Mrengo huo ambao unashirikisha vyama tofauti vya kisiasa umeweka masharti makali kwa wawaniaji ambao wanataka uungwaji mkono wake kwa nyadhifa kama ugavana, useneta na ubunge.

“Tutamuunga mkono tu mwaniaji ambaye yuko tayari kutujumuisha katika serikali ijayo. Hii ni kinyume na awali ambapo tulinyimwa nafasi hiyo licha ya mchango tuliotoa katika kuwashinikiza wapigakura kujitokeza,” akasema Bw Dennis Mugo, aliyewania udiwani katika wadi ya Huruma, Uasin Gishu mnamo 2017 kwa tiketi ya Chama cha Jubilee (JP).

Kundi hilo liliviomba vikosi vya usalama kubaini maeneo yanayoweza kukumbwa na ghasia na kuchukua hatua za mapema kuzuia mapigano kutokea.

Liliomba vikosi hivyo kuwachukulia hatua kali wale watakaobainika kueneza chuki za kikabila na kisiasa miongoni mwa wenyeji.

“Kama mrengo wa kisiasa wenye maono, tumeweka kura zetu pamoja ili kuimarisha ushawishi wetu. Tunataka uwepo wa chaguzi zenye amani kinyume na kitambo ambapo eneo hili limekuwa lilikumbwa na ghasia kila wakati,” akasema Bw Andrew Sure kutoka ODM katika eneo la Uasin Gishu.

Kundi liliomba ugavi sawa wa raslimali. Lilitaja hali ambapo upande unaoshinda hutwaa kila kitu kama chanzo cha taharuki ya kisiasa ambayo huzuka kila baada ya uchaguzi.

“Kama wakazi, tunataka kubadili mtindo ambapo wale wanaoshindwa kwenye chaguzi huwa wanakosa kujumuishwa kwenye masuala muhimu kama basari, utoaji tenda na mipango mingine ya maendeleo na wanaoibuka washindi,” akasema Bi Pamela Arunga kutoka chama cha ANC.

You can share this post!

Vita vya ubabe kati ya gavana, Wetang’ula mazishini

FA yashtumu tukio la ubaguzi wa rangi dhidi ya Saka, Sancho...