• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 5:55 PM
Vyama vidogo vinachochea chuki na ukabila, Ruto adai

Vyama vidogo vinachochea chuki na ukabila, Ruto adai

NA KIPKOECH CHEPKWONY

NAIBU Rais Dkt William Ruto Jumatatu amewataka wapinzani wake, akiwemo kinara wa ODM Raila Odinga, kukataa kuungana na vyama vidogo anavyodai ni vya kikabila.

Dkt Ruto aliyekuwa akizungumza katika msururu wa mikutano ya kisiasa kwenye Kaunti ya Nyamira, alisema vyama vidogo vinaendeleza ukabila nchini.

Kiongozi huyo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) alionekana kuwashambulia baadhi ya viongozi wa eneo la Kisii ambao mwezi uliopita walizindua chama chao cha United Progressive Alliance (UPA).

UPA, ambayo inahusishwa na Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i tayari imetangaza kumuunga mkono kiongozi wa chama cha ODM Bw Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Dkt Ruto ameshikilia kuwa chama chake cha UDA hakitafanya muungano na chama chochote kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Kwa upande mwingine, Bw Odinga anaonekana kukumbatia vyama vidogo. Kuna zaidi ya vyama vya kisiasa 90 humu nchini, huku vyama vingine zaidi ya 20 vikipewa vyeti vya muda huku vikisubiri kuidhinishwa kuwa vyama halisi.

Jumatatu, Dkt Ruto alisema vyama vidogo vinachochea uhasama wa kikabila hivyo kutishia amani nchini.

“Wanasiasa wa upinzani wanadai kuwa wanataka kuunganisha nchi ilihali wanazunguka kila mahali na vyama vidogo vya kisiasa. Watawezaje kuunganisha nchi?” akauliza Dkt Ruto.

Naibu Rais aliwataka Wakenya kutokubali kugawanywa na wanasiasa kwa misingi ya kikabila. Aliongeza kuwa vyama vya kisiasa vya kikabila vinazua migawanyiko na chuki miongoni mwa Wakenya.

“Hatutakubali kurejeshwa nyuma katika siasa za kikabila,” akasema.

Wakati huo huo, Naibu wa Rais aliwahimiza vijana wajiandikishe kuwa wapigakura ili wachague viongozi ambao watashughulikia masilahi yao,  ikiwemo ukosefu wa ajira.

“Vijana mnapaswa kujua kwamba siasa zinahusu maslahi, mnnafaa kupigia kura serikali ambayo itashughulikia mahitaji yenu,” alisema.

Wabunge waliokuwa katika mkutano huo ni pamoja na Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi), Shadrack Mose (Kitutu Masaba), Dominic Koskei (Sotik), Vincent Musyoka (Mwala), Joash Nyamoko (Mugirango Kaskazini), waliokuwa wabunge Omingo Magara, Walter Nyambati na Joseph Kiangoi.

Viongozi hao walisema  kuwa Wakenya wanapaswa kuruhusiwa kuchagua viongozi wanaowakilisaha na kutetea haki zao bila kushurutishwa.

Mbunge wa Mugirango Kusini, Sylvanus Osoro, alisema kuwa Wakenya wengi wanataka mabadiliko kwa vile utawala wa sasa umekengeuka kinyume na ajenda yake ya awali.

Bw Kemosi alimtaka Rais Kenyatta kuzingatia kukamilisha mipango yake ya urithi. “Tunamwomba Rais awape Wakenya nafasi ya kumchagua kiongozi wapendao bila kuingiliwa,” akasema Bw Kemosi.

Aidha Bw Osoro alimshauri Rais Uhuru Kenyatta aache wakenya wafanye uamuzi wao wenyewe bila kuingiliwa kuhusiana na  viongozi wanaowataka  ifikapo wakati mwafaka wa uchaguzi.

“Tunataka Wakenya wamchague kiongozi wamtakaye na ambaye ana uwezo wa kubadilisha uchumi kando na kushughulikia ukosefu wa ajira kwa vijana,” Bw Musyoka akasema.

“Hatutakubali kurejeshwa katika siasa za ukabila na ukabila zinazochochea mifarakano miongoni mwa Wakenya,” Dkt Ruto aliongezea.

You can share this post!

Serikali yawataka wazazi kuwakataza watoto kutazama Squid...

ODM Magharibi wataka tiketi ya Raila-Oparanya

T L